1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHungary

Bunge la Hungary laidhinisha ombi la Sweden kujiunga na NATO

27 Februari 2024

Bunge la Hungary limepiga kura na kuidhinisha ombi la Sweden la kujiunga na muungano wa kujihami wa mataifa ya Magharibi NATO.

https://p.dw.com/p/4cv41
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban akilihutubia bunge baada ya wabunge kuidhinisha ombi la Sweden la kujiunga na NATO.
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban akilihutubia bunge baada ya wabunge kuidhinisha ombi la Sweden la kujiunga na NATO.Picha: Denes Erdos/AP Photo/picture alliance

Muswada huo ulipitishwa kwa kura 118 za "Ndio" huku kukiwa na kura sita za "Hapana".

Kura hiyo imefanyika baada ya kucheleweshwa kwa zaidi ya miezi 18 kufuatia mzozo na washirika wa Hungary waliojaribu kuishawishi serikali mjini Budapest kuondoa kizuizi chake kwa uanachama wa Sweden.

Taifa hilo la ukanda wa Nordic lilituma ombi la kujiunga na NATO miezi michache tu baada ya Urusi kuivamia Ukraine mnamo mwaka 2022.

Kila nchi mwanachama wa NATO inahitajika kuridhia ombi la mwanachama mpya kujiunga na muungano huo wa ulinzi na Hungary ilikuwa nchi ya mwisho kati ya wanachama 31 kuidhinisha ombi la Sweden.

Uamuzi wa Hungary unafungua njia ya utanuzi wa NATO kuelekea mashariki katika muda wa mwaka mmoja.

Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson amesema ilikuwa siku ya "kihistoria" na hatua kubwa kwa taifa hilo kuachana na miaka 200 ya kutoegemea upande wowote.

Finland pia ilikumbana na vizuizi kadhaa katika ombi lake la uanachama na hatimaye ilijiunga na NATO mnamo mwezi Aprili mwaka jana.