Hungary: Je Orban ana tatizo gani na Ukraine?
16 Desemba 2022Tangu mwanzo, rais wa Hungary Victor Orban na serikali yake wamechelea kulaani uchokozi wa Urusi kama itakikanavyo kulingana na sheria ya kimataifa.
Hadi leo Orban huutaja kuwani "vita vya Urusi na Ukraine”. Mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa "hivyo si vita vyao” na kwamba ni mzozo ambao pande husika zinapaswa kusuluhisha wenyewe. Pamoja na masuala mengine swali linaloulizwa ni je Orban ana shida gani na Ukraine.
Kwa miezi kadhaa, kulikuwa na minong'ono ikiwa kweli Hungary itazuia mpango wa Umoja wa Ulaya kuipa Ukraine euro bilioni 18. Kwa muda huo wote wanasiasa wengi wa Ulaya walifikiri Orbanban alikuwa akitania.
Hungary yazuia msaada wa kifedha wa EU kwa Ukraine
Lakini mnamo Disemba 6, Orban alithibitisha kitisho chake kwa kuzuia mkopo huo wa kifedha mjini Brussels. Muda mchache baadaye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba Hungary imetumia kura yake ya turufu kuzuia mkopo huo. Lakini katika hali ya kukanganya Zaidi aliongeza kuwa "hii ni Habari ya uwongo […] hakuna kura ya turufu, hakuna hujuma.” Alisema pia kwamba Hungary ipo tayari kuisaidia Ukraine kwa misingi ya nchi mbili.
Iwe ilikuwa kura ya kweli ya turufu au la, hatua ya Hungary kuzuia msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Ukraine ndiyo tukio baya zaidi la hivi karibuni kati ya nchi hizo ambazo uhusiano wao si mzuri.
Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februar 24, kumekuwa na misururu ya hali mbaya kama hizo.
Msimamo wa Orban kuhusu vikwazo vya EU kwa Urusi
Japo kwa muda mrefu Hungary imekuwa ikivumilia vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, ilipinga mpango wa kumwekea vikwazo Patriarch Kirill ambaye ni mkuu wa kanisa la Orthodox nchini Urusi lakini ambaye pia ni mchochezi wa vita.
Maoni: Viktor Orban anaudhihaki Umoja wa Ulaya
Orban hata hivyo amefanya makubaliano ya kuiondoa nchi yake kwenye maamuzi ya pamoja ya kususia mafuta ya Urusi. Mara kwa mara amekosoa pia vikali baadhi ya vikwazo dhidi ya Urusi. Kwa hakika kwa sasa, serikali ya Budapest inaendesha kampeni inayoukosoa Umoja wa Ulaya kwa kuharibu uchumi wa Hungary kutokana na vikwazo dhidi ya Urusi.
Zaidi ya hayo ni kwamba Orban amepinga msaada wa silaha kupelekewa Ukraine kwa kukataa silaha hizo zisisafirishwe kupitia nchi yake.
Swali kuu ni je, tatizo la Orban dhidi ya Ukraine ni lipi?
Kumekuwa na hisia za kutoridhisha kati ya Hungary na Ukraine- kwa sababu ya Wahungary wachache walioko Transcarpathia, magharibi mwa Ukraine.
Wakati Orban alichukua hatamu za kuwa Waziri mkuu mwaka 2010, kulikuwa na Wahungary wasiozidi 200,000 waliokuwe katika jimbo hilo. Lakini leo hii, idadi hiyo imepungua hadi 130,000.
Budapest haikufurahishwa pia na mpango wa kubadilisha lugha ya Ukraine ambayo kimsingi ilikusudia kupunguza ushawishi wa lugha ya Kirusi nchini Ukraine. Serikali ya Orban ilihisi mpango huo uliwalenga pia Wahungary wachache walioko Ukraine.
Wiki chache tu baada ya Urusi kuchukua rasi ya Crimea mwaka 2014, Orban alitaka rasi hiyo kujitegemea, wakaazi waruhusiwe uraia pacha wakiwemo Wahungary walioko huko. Matamshi yake yalishutumiwa na kutajwa kuwa ya kuhimiza utengano.
Kwa ujumla sera ya Orban kuelekea Ukraine haichochewi na nchi yenyewe bali mivutano ya ndani na vipaumbele katika sera ya kigeni.
Mwandishi: Keno Verseck
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Daniel Gakuba