1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden na Putin wasifu mazungumzo yao mjini Geneva

17 Juni 2021

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wamesema mkutano wao wa mjini Geneva ulikuwa wa mafanikio na wamezungumzia uwezekano wa mataifa hayo mawili kurekebisha dosari na kufanya kazi pamoja.

https://p.dw.com/p/3v4Gk
Schweiz l Biden und Putin treffen sich in Genf l Begrüßung
Rais Joe Biden wa Marekani (kulia) alipokutana na Vladimir Putin wa Urusi mjini Geneva.Picha: Patrick Semansky/AP/picture alliance

Viongozi hao wawili wameutumia mkutano wao wa kwanza mjini Geneva kujaribu kupunguza mivutano inayoyumbisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Baada ya mazungumzo ya karibu saa tatu Biden na Putin walijitokeza mbele ya umma wakiwa na sura za bashasha kila mmoja akisema mkutano kati yao ulikuwa wa mafanikio.

Rais Putin aliwaambia waandishi habari kuwa mazungumzo yalikuwa ya "kujenga" na kuongeza kuwa wamekubaliana kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kwa kuanza wanawarejesha kazini mabalozi wanaowakilishi nchi zao mjini Moscow na Washington.

Kwa upande wake Biden ameutaja mkutano huo na Putin uliofanyika kwenye hoteli moja ya fahari pembezoni mwa ziwa Geneva kuwa "mzuri".

Biden ambaye alikuwa anahitimisha ziara yake muhimu barani Ulaya, amesema yeye na Putin wamejadili uwezekano wa kufanya kazi pamoja  kwenye masuala ambayo mahasimu hao wawili wana maslahi yanayofanana ikiwemo kuhusu Iran, Syria na utafutaji rasimali kwenye eneo la Aktiki.

Biden aliwaambia waandishi habari kuwa madola hayo mawili yenye nguvu "yana wajibu wa aina yake" katika uga wa kimataifa.

Biden aionya Moscow kuhusu mashambulizi ya mtandao

Hata hivyo, Biden amesema ameutumia mkutano huo kuikanya Kremlin dhidi ya mashambulizi ya mtandao akisema huo ni mstari mwekundu kwa Washington kwa sababu mifumo yake ya kompyuta imeorodheshwa kuwa moja ya miundombinu muhimu sana kwa taifa hilo.

USA-Russland-Gipfel in Genf | Joe Biden
rais Joe Biden wa Marekani akizungumza na waandishi habari mjini Geneva.Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Amemtaka Putin kufanya awezalo kuzuia mashambulizi hayo ya mtandao akitahadharisha kuwa Marekani itajibu vikali iwapo hilo litakiukwa.

Kwa sehemu fulani Washington imekuwa ikiitwika jukumu Moscow kwa kuyahifadhi magenge ya uhalifu wa mtandao na kwa shambulizi la hivi karibuni la mtandaoni la SolarWinds lililozilenga taasisi chungunzima za Marekani.

Masharika ya kijasusi ya Marekani pia yameituhumu Urusi kwa kuendesha kampeni chafu ya kujaribu kuingilia na kuvuruga chaguzi mbili za rais nchini Marekani.

Kama ilivyotarajiwa eneo jingine lililojadiliwa lilikuwa ni suala la udhibiti wa silaha nzito na viongozi hao wamekubaliana kuandaa mashauriano ya ngazi ya juu kuhusu suala hilo.

Biden amesema hakuna mashaka kwamba Putin hana mpango wa kurejea enzi ya vita baridi ambapo madola hayo mawili yalitunishiana misuli kutokana na uwezo mkubwa wa kijeshi kutokana na ule ukweli kwamba kila upande una hazina ya silaha za nyuklia.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa nchi hizo mbili kubadilishana wafungwa, rais Putin alisema yeye na Biden wameweka wazi uwezekano wa hilo kufanyika lakini hakufafanua iwapo kuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa.

Suala la Navalny na Haki za Binadamu pia vilizungumzwa

Schweiz l Biden und Putin treffen sich in Genf l PK Putin
Rais Vladimir Putin wa Urusi akizungumza na waandishi habari mjini Geneva Picha: Denis Balibouse/AFP

Ama kuhusu suala la Haki za Binadamum rais Putin amesema Biden aliliweka mezani wakati wa mazungumzo lakini hakuna mwafaka wa pamoja uliopatikana. Baadae rais Biden alisema alilitaja waziwazi suala hilo ikiwemo juu ya kuandamwa kwa kiongozi wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny.

Mkutano kati  ya Biden na Putin umefanyika katika wakati mahusiano baina ya Moscow na Washington yamepwaya kwa kiwango cha chini kabisa hususani tangu rais Biden alipoingia madarakani mnamo mwezi Januari.

Pale Biden alipomfananisha Putin na "muuaji", Urusi ilichukua uamuzi wa nadra mnamo mwezi Machi kwa kumrudisha nyumbani Balozi wake nchini Marekani Anatoly Antonov na Washington nayo ilimtaka Balozi wake kuondoka mjini Moscow.

Baada ya mkutano wa mjini Geneva wengi watasubiri kuona kile kitakachotokea katika mahusiano baina ya mafahali hao wawili na kutazama iwapo zawadi ya miwani meusi na picha ya nyati aliyoitoa Biden kumpatia Putin mwishoni mwa mazungumzo itasaidia chochote katika kujenga urafiki na kuaminiana.