Biden na Putin wakubali mabalozi kurudi Washington, Moscow
16 Juni 2021Hii ni kufuatia mazungumzo kati yake na rais mwenzake wa Marekani Joe Biden mjini Geneva Jumatano.
”Watarudi katika maeneo yao ya kazi. Kuhusu lini, nalo ni swali jingine la kiufundi,” aliwaambia waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wao.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Moscow na Washington umekuwa mbayá.
Mnamo mwezi Machi, Biden alimfananisha Putin na "muuaji”. Urusi ilichukua hatua isiyo ya kawaida kumuita balozi wake Anatoly Antonov na vilevile kuamuru balozi wa Marekani nchini Urusi John Sullivan arudi Washington.
Biden na Putin wakutana katika mkutano wa kilele wakati nchi hizo mbili zikiwa hazikubaliana kwenye masuala mengi.
Sulivan aliondoka Moscow mnamo mwezi Aprili wakati nchi hizo zilipotangaza vikwazo vya kulipizana kisasi pamoja na kuwatimua wanadiplomasia.
Mnamo mwezi Mei, Urusi ililiorodhesha rasmi Marekani kama taifa ‘lisilo rafiki' linalozuia ubalozi wake kuwaajiri raia wa Urusi. Taifa jingine pekee kwenye orodha hiyo ni Jamhuri ya Czech.
Biden na Putin wakutana Geneva
Vilevile Biden na Putin wamekubaliana kurudi kwenye meza ya mazungumzo kuhusu udhibiti wa silaha.
Mkutano huo wa kilele kati ya viongozi hao ulidumu kwa muda wa chini ya saa nne, tofauti na ilivyotarajiwa kama ambavyo washauri wao walisema awali.
Licha ya mazungumzo yao, viongozi hao hawakuhutubia waandishi wa habari wakiwa pamoja, bali kila mmoja alizungumza na waandishi wa habari kivyake. Putin ndiye alikuwa wa kwanza kuzungumza na waandishi habari punde baada ya mkutano wao kumalizika.