Biden na Putin wajadili mahusiano ya Washington na Moscow
27 Januari 2021Kulingana na Ikulu ya Marekani, wakati wa mazungumzo hayo rais Biden, amemweleza Putin juu ya wasiwasi alionao kuhusu kukamatwa kwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Urusi Alexei Navalny, tuhuma kuwa Moscow ilihusika na shambulizi la mtandao la hivi karibuni dhidi ya Marekani na madai kwamba Urusi imewalipa wanamgambo kuwauwa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.
Kwa upande wa Ikulu ya Kremlin yenyewe taarifa yake imejikita kuzungumzia majibu ya Putin kwa pendekezo la Biden la kurefusha mkataba kati ya Marekani na Urusi wa kudhibiti silaha nzito unaofahamika kama New START.
Ijapokuwa taarifa kutoka Washington na Moscow zimetilia uzito mambo tofauti, pande zote lakini zimeashiria kwamba mahusiano kati ya Urusi na Marekani walau katika siku za mwanzo za utawala wa Biden yataongozwa na shauku ya kutochochea mivutano lakini vilevile bila ya kuharakisha kumaliza tofauti zilizopo baina ya mataifa hayo hasimu tangu enzi ya vita baridi.
Kuhusu suala la mkataba wa New START marais hao wawili wamekubaliana wajumbe wa kila upande wakamilishe haraka makubaliano ya kurefusha kwa miaka mitano utekelezaji wa mkataba huo wakati muda wa sasa utakapofikia mwisho mnamo mwezi unaokuja.
Biden analenga kumkabili Putin
Utawala wa rais aliyondoka madarakani nchini Marekani Donald Trump ulikwishajitoa kutoka mikataba miwili muhimu ya kudhibiti silaha kati ya nchi hiyo na Urusi na uliazimia kutorefusha muda wa mkataba wa New START.
Ingawa viongozi hao wawili wamekubalina kurefusha mkataba huo, ikulu ya White House imesema rais Biden amemweleza waziwazi rais Putin kuwa nchi yake inaunga mkono uhuru wa Ukraine wakati Urusi inawaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga mashariki ya nchi hiyo.
Biden pia aliweka mezani tuhuma za kuhusika kwa Urusi kwenye shambulizi baya kabisa la mtandao maarufu SolarWinds lililozilenga idara za usalama za Marekani na ripoti kwamba Moscow inatoa fedha kwa wanamgambo wa Taliban kuwauwa wanajeshi wa Marekani walioko Afghanistan.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jen Psaki amesema nia ya Biden "ilikuwa ni kuweka wazi kwamba Marekani itachukua hatua nzito kulinda maslahi yetu ya taifa na katika kujibu vitendo vya chokochoko vya Urusi"
Suala la Navalny lawajumuishwa kwenye mazungumzo
Ama kuhusu suala la mkosoaji wa serikali ya Urusi Alexei Navalny Biden amemweleza Putin kuwa hakubaliani na jinsi serikali yake inavyomuandama kiongozi huyo wa upinzani.
Mazungumzo hayo ambayo ni ya kwanza tangu kuapishwa kwa Biden yamefanyika wakati rais huyo mpya wa Marekani analenga kubadili sera ya nchi yake kwa kuchukua msimamo mkali kuelekea Urusi baada ya mtangulizi wake Donald Trump kujivutavuta kumkabili moja kwa moja rais Putin.
Katika hatua nyingine, Biden pia amezungumza na katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg na kurejea azma ya utawala wake ya kuimarisha ushirika huo wa kijeshi kati ya Washington na mataifa ya Ulaya.