Marekani yajiondoa kwenye mkataba wa silaha
1 Februari 2019Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo ametangaza kuwa Marekani inajitoa kwenye mkataba kati ya Marekani na Urusi wa kuzuia urundikiaji wa silaha tangu kumalizika kwa Vita Baridi.
Kujiondoa kwa Marekani kumekuwa kukitarajiwa kwa miezi kadhaa. Hatua hiyo imetokana na mzozo ambao haujasuluhishwa kwa miaka mingi wa madai kuwa Urusi imekuwa ikikiuka mkataba huo ulioafikiwa mwaka 1987 ambao unapiga marufuku baadhi ya makombora ya kufyatuliwa ardhini. Urusi imekana madai ya kukiuka mkataba huo.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo amesema Marekani itajitoa kwenye mkataba huo kesho Jumamosi, akiongeza kuwa ikiwa Urusi haitarudi katika njia ya kuheshimu utekelezwaji wa mkataba huo, basi utavunjika. Pompeo ameeleza kuwa:
''Tuliipa Urusi muda wa kutosha wa kurekebisha mienendo yake na kujitolea kikamilifu kuheshimu mkataba wa INF. Muda huo unamalizika kesho lakini Urusi imekataa kuchukua hatua yoyote ya kurejesha hali halisi na inayoweza kuthibitishwa ya kuheshimu mkataba katika kipindi cha siku 60 tulizoipa. Kwa hivyo kuanzia kesho, Jumamosi, Marekani itajiondoa kwenye mkataba huo''
Maafisa wa Marekani wameelezea wasiwasi kuwa China ambayo si mwanachama wa mkataba huo, imekuwa ikijiwekea makombora mengi barani Asia, hatua ambayo Marekani haiwezi ikazuia kwa sababu ya mkataba huo.
Pompeo ameongeza kuwa nchi yake ingali inataka kushiriki katika mazungumzo na Urusi kuhusu udhibiti wa silaha na inatumai Urusi itaheshimu utekelezwaji wa mkataba huo
Madai dhidi ya Urusi yametokana na hatua ya Urusi kutengeneza makombora ya ardhini aina ya 9M729, lakini ambayo Urusi inashikilia kuwa hayana uwezo wa kufyatuliwa kupita umbali unaokubaliwa na mkataba huo.
Mapema mwezi Disemba, mwaka uliopita, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza kuwa Marekani ingeipa Urusi siku 60 kurejea katika hali ya kuuheshimu mkataba huo, kabla iipe notisi rasmi ya kujiondoa hatua ambayo itakamilika baada ya miezi sita.
Mkataba huo ambao pia unajulikana kwa Kiingereza kama Intermediate-Range Nuclear Forces (INF), ulikuwa hatua ya kwanza ya kupiga marufuku kabisa aina ya makombora ya ardhini yanayoweza kufyatuliwa umbali wa kati ya kilomita 500 hadi kilomita 5,500.
Kuachana na mkataba wa INF kutauruhusu utawala wa Trump kuikabili China japo haijabainika wazi ni vipi utafanya hivyo.
Mhariri: Josephat Charo