Biden asema hang'oki licha ya makosa ya aibu
12 Julai 2024Msimamo wake ulijiri wakati miito ya kumtaka kusitisha kampeni ikiongezeka, ambapo wabunge 17 wa chama cha Democratic wamejitokeza wazi na kumhimiza rais huyo mwenye umri wa miaka 81 kuachana na kampeni.
Katika mkutano muhimu na waandishi wa habari mwishoni mwa mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington, Biden alikiri ipo haja ya kutuliza hofu miongoni mwa Wanademokrati lakini akasisitiza dhamira yake ya kuendelea na kampeni, na kusema hayumo kwenye kinyang'anyiro hicho kwa ajili ya urathi wake.
"Siko katika hili kwa ajili ya urathi wangu. Niko katika hili kukamilisha kazi niliyoanza," Biden alisema. "Ratiba yangu imekuwa ya kuchosha kwa hivyo nikipunguza kasi na siwezi kufanya kazi hiyo, hiyo ni ishara kwamba sitakiwi kuifanya. Lakini bado hakuna dalili ya hilo. Hakuna."
Hata hivyo juhudi za kujionyesha kama kiongozi alie imara bado zilitiwa doa na hatua yake ya awali alipomtambulisha Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kama adui yake wa Urusi Vladmir Putin, na kisha kumtaja Makamu wa Rais Kamala Harris kama "Makamu wa Rais Trump" kwenye mkutano wa habari wa NATO.
Kampeni ya Biden imekumbwa na mgogoro tangu alipoboronga kwenye mdahalo wa televisheni dhidi ya Trump wiki mbili zilizopita, na kuibua wasiwasi mpya kuhusu umri wake-- na mkutano huo wa waandishi habari uliodumu kwa karibu saa nzima, ulikusudiwa kuonyesha kwamba bado anao uwezo.
Rais huyo amekabiliwa na wito unaoongezeka wa Wademokrat kuachana na kampeni yake, wakihofia kwamba Trump atamshinda kwa urahisi, na idadi hiyo iliongezeka baada ya mkutano wa wa jana ambapo mpaka sasa wabunge 17 wa chama hicho wamjitokeza wazi wazi kumtolea wito Biden aachane na kampeni.
Majaribio ya uwezo wa Harris kuchukua mikoba
Biden aliweka wazi kuwa anamuunga mkono Harris -- ambaye kama makamu wa rais angechukua nafasi yake katika hali ya dharura, lakini pia anaonekana na idadi inayoongezeka ya Wanademokrat kama mgombea mwenye nguvu kwa tiketi ya chama hicho.
Huku kukiwa na ripoti kwamba timu ya kampeni ya Biden inapima kimya kimya nguvu ya Harris katika mchuano wa kinadharia dhidi ya Trump, rais huyo alisema asingemchagua kuwa makamu wake kama asingekuwa na uwezo wa kuwa rais.
Soma pia: Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka
Pia alikanusha ripoti kwamba alihitaji kulala ifikapo saa mbili usiku, wakati ambao alikuwa bado akifanya mkutano wake na wanahabari siku ya Alhamisi.
Lakini baada ya kulaumu utendaji mbaya katika madahalo kwa mchanganyiko wa uchovi wa safari za ndege na baridi, alikiri kwamba itakuwa "ni jambo la busara kwangu kujiweka sawa kidogo."
Alisisitiza pia kwamba uchunguzi wa mishipa ya fahamu ulionyesha alikuwa katika "hali nzuri" na kusema angechukua vipimo vingine ikiwa madaktari wake watapendekeza hivyo, lakini bado hawajafanya hivyo.
Sera ya kigeni na uwezo wa kuwashughulikia Putin na Xi
Biden pia alijibu msururu wa maswali kuhusu sera ya kigeni na ya ndani yenye majibu ya kina ambayo wakati mwingine yalipotoka, huku akichanganya Ulaya na Asia.
Huku maswali yakiulizwa juu ya uwezo wake wa kushikilia msimamo wake dhidi ya viongozi wa kiimla kama Putin au Xi Jinping wa China, Biden alisema yuko "tayari kukabiliana nao sasa na miaka mitatu kuanzia sasa."
Hata hivyo utendakazi wake wa uhakika ulishindwa kuzuia wasiwasi, huku wabunge watatu zaidi wa chama cha Democratic wakimtaka aache kinyang'anyiro hicho, na kufikisha jumla ya 17.
Wakati huo huo Trump alimdhihaki Biden kuhusiana na makosa yake wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Mdanganyifu Joe anaanza mkutano wake na waandishi wa habari wa 'Big Boy' na, 'Nisingemchagua Makamu wa Rais Trump kuwa makamu wa rais... Kazi nzuri, Joe!" Trump aliandika kwenye mtandao wake wa Kijamii wa Truth Social.
Viongozi wa NATO wamuunga mkono Biden
Ikulu ya White House iliutaja kama mkutano wa "Big Boy" ikiwa ni mara ya kwanza kwa Biden kuonekana peke yake, bila maandishi ndani ya miezi minane -- huku kukiwa na shutuma kwamba uzee wake umemzuwia kuonekana mbele ya umma.
Wasiwasi juu ya afya ya Biden ulizidishwa na kosa la lake kwenye jina la Zelensky, ambalo lilizusha minong'ono ndani ya chumba cha mkutano. Zelensky, kiongozi wa wakati wa vita wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi 2022, alicheka.
Soma pia: Mamilioni ya Wamarekani kufuatilia mdahalo wa Televisheni kati ya Joe Biden na Donald Trump
Viongozi wenzake katika mkutano wa NATO walijibu maswali kuhusu utimamu wake na majibu yao yalikuwa yanamuunga mkono kwa ujumla. "Kuteleza kwa ulimi hutokea," Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema Biden alionekana imara wakati wa mkutano, huku Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer akisema "alikuwa katika hali nzuri."
Mchuano mkali kati ya Biden na Trump
Lakini waungaji mkono muhimu wa Marekani wamejitenga na maneno ya kupamba ya kidiplomasia.
Muigizaji wa Hollywood na mfadhili wa chama cha Democratic George Clooney alitoa wito kwa Biden kuondoka kwenye kinyang'anyiro, na bibi wa chama Nancy Pelosi alisita kumuunga mkono kikamilifu.
Kura ya maoni iliyotolewa Alhamisi ilionyesha zaidi ya nusu ya Wanademokrasia wanasema Biden anapaswa kusitisha azma yake ya kuwania muhula wa pili, na theluthi mbili ya Wamarekani wanaamini anapaswa kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Biden na Trump wanaendela kukaribiana sana kwenye uungwaji mkono wa umma kwa asilimia 46-47 mtawalia, kulingana na uchunguzi uliofanywa na shirika la uchunguzi wa maoni la Ipsos kwa niaba ya mashirika ya Washington Post na ABC News.
Chanzo: Mashirika