1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo la Biden kutowania tena urais laongezeka

9 Julai 2024

Rais Joe Biden wa Marekani leo Jumapili amerejea kwenye ulingo wa kampeni akinuwia kuinusuru nafasi yake ya kugombea muhula wa pili katika wakati shinikizo linaongozeka kumtaka asiwe mgombea kwenye uchaguzi wa Novemba.

https://p.dw.com/p/4hz5I
Rais Joe Biden wa Marekani
Rais Joe Biden wa Marekani Picha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 anamaliza wiki hii na kufungua wiki nyingine ngumu kwa mikutano miwili kwenye jimbo lenye ushindani mkubwa la Pennsylvania.

Kisha mwanzoni mwa wiki atawakaribisha viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa mkutano wa kilele mjini Washington.

Yote hayo yanamgonja wakati akiwa katikati ya shinikizo la kumtaka aachane na mipango ya kuwania muhula wa pili madarakani baada ya kufanya vibaya kwenye mdahalo wake dhidi ya Donald Trump uliofanyika mwezi uliopita.

Kupwaya kwa Biden kwenye mdahalo huo kumeleta hamkani ndani ya chama chake cha Democratic na miito ya kumtaka akae pembeni inatoka kila upande.

Wengi wana wasiwasi na umri wake mkubwa na uwezo wake wa kimwili na kiakili wa kuwa rais kwa miaka mingine minne.

Mwenyewe asema yuko imara kushinda uchaguzi wa Novemba

Hata hivyo mwenyewe amekaidi shinikizo linalomkabili akisema yuko imara kuitumikia Marekani na kwamba yeye ndiye mgombea pekee anayeweza kumshinda Donald Trump inayeaminika ataidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa chama cha Republican.

Mdahalo kati ya Biden na Trump
Rais Joe Biden wa Marekani na Donald Trump walipochuana kwenye mdahalo wa televisheni mnamo Juni 27, 2024. Picha: Brian Snyder/REUTERS

"Nilimshinda Trump mwaka 2020. Nitamshinda tena mwaka huu 2024," amesema Biden kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii katika chapisho lililoweka siku ya Jumapili.

Licha ya juhudi zake za kuonesha kwamba anao uwezo wa kushinda uchaguzi, mashaka bado hayajapungua.

Siku ya Ijumaa Biden alifanya mahojiano na kituo cha televisheni cha ABC akilenga kuonesha uwezo wake wa kuzungumza na kujenga hoja lakini wengi wanasema mahojiano hayo hayakusaidia chochote.

Kihunzi chake kikubwa kinachokuja mbele ya macho ya umma itakuwa ni mkutano na waandishi habari uliopangwa Alhamisi ijayo wakati wa mkutano wa NATO.

´Uasi´ dhidi ya Biden waanza kusambaa ndani ya chama cha Democratic 

Mahojiano ya Biden na kituo cha ABC
Mahojiano aliyoyafanya Joe Biden kujaribu kutuliza wasiwasi wa wapiga kura.Picha: ABC via Getty Images

Hadi sasa wabunge watano wa Democratic wamemtaka waziwazi Biden ajiengue na miito ya aina hiyo inaongezeka.

Seneta wa chama cha Democratic Chris Murphy, ambaye ni mwandani wa Biden, amesisitiza kwamba anaamini Biden ataweza kusawazisha upepo mbaya unaovuma na hata kushinda uchaguzi. Lakini amesema "rais itafaa afanye zaidi ya sasa," ikiwemo kushiriki mihadhara ya wazi itakayomkutanisha na wapigakura tena bila kutoa hotuba iliyoandikwa.

Amesema matukio kama hayo yatawahakikishia wapigakura juu ya uwezo wake wa kimwili na kiakili wa kuhudumu muhula wa pili madarakani.

Maoni hayo ya Murphy ameyatoa wakati kiongozi wa wabunge wa Democratic ndani ya Baraza la Wawakilishi Hakeem Jeffries ameandaa mkutano kwa njia ya mtandao na wabunge wa chama hicho kujadili hatua za kuchukua na kusonga mbele kuhusu hali ya Biden.

Maseneta wa Democratic inaarifiwa nao pia wanatayarisha kikao kama hicho.