Biden: 'Karibu tuipoteze Marekani'
6 Januari 2024Rais Joe Biden ametoa hotuba hiyo katika mkesha wa kumbukumbu ya uvamizi huo, Januari 6, 2021 baada ya wafuasi wa Trump kuvamia jengo la Capitol Hill ambako wabunge walikuwa wakiidhinisha ushindi wake wa urais.
Biden amesema kampeni za Trump ziligubikwa na maslahi binafsi kuliko kuwasaidia Wamarekani na kwamba rais huyo wa zamani anaweza kuitoa muhanga demokrasia ikiwa atarejea madarakani.
Biden: 'Nilishinda uchaguzi, alishindwa'
"Nilishinda uchaguzi, na alishindwa," Biden alisema, "Alibakiwa na chaguo moja, machafuko ya Januari 6."
Rais huyo wa sasa wa Marekani amesema uvamizi katika jengo la Capitol ulikuwa ni "siku ambayo wangekaribia kuipoteza Marekani."
Soma pia: Biden amlaumu Trump kwa uvamizi wa Capitol
Biden ametoa hotuba hiyo katika eneo la Valley Forge, ambako kihistoria panarudisha kumbukumbu ya mahali ambako aliyekuwa rais George Washington na jeshi la muungano wa Makoloni "Continental Army" walikaa kwa miezi sita chini ya mazingira magumu na baridi kali wakati wa vita vya Mapinduzi ya Marekani miaka 250 iliyopita. Biden alizungumzia juu ya vitisho dhidi ya demokrasia, baada ya majadiliano na wanahistoria na wasomi katika Ikulu ya White House
Biden amesema kwambaTrump aliyasifu machafuko hayo ya Capitol yaliyosababisha watu karibu tisa kufa, ama wakati wa machafuko au baada ya kisa hicho na kuongeza kuwa "kwa kuangazia tukio hilo la Januari 6, Trump anajaribu kuiiba historia kana alivyojaribu kuiba kura."
"Kampeni za Donald Trump zilikuwa ni kwa ajili yake, " alisema Biden akiiangazia mipango ya Trump ya kulipiza kisasi dhidi ya maadui zake wa kisiasa ikiwa atarejea ikulu ya White House. "Sio Marekani. Sio wewe. Kampeni za Donald Trump zinazungumzia tu yaliyopita, na sio ya siku za usoni."
Biden dhidi ya Trump; awamu ya pili
Bado haiko wazi ikiwa maonyo hayo ya Biden yatakuwa na matokeo yoyote kwa wapiga kura wakati kampeni za urais zikianza.
Biden alimshinda Trump kwa asilimia 51.3 ya kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, lakini ongezeko la mfumuko wa bei na wasiwasi kuhusiana na umri wake mkubwa kwa pamoja vinaibua mashaka hata zaidi kwa wafuasi wake.
Trump kwa upande wake anatarajia kufanya mkutano wa hadhara huko Iowa siku ya Jumapili.
Soma pia: Trump apigwa marufuku kushiriki uchaguzi wa mchujo katika jimbo la Maine
Trump anakabiliwa na msururu wa kesi, ikiwa ni pamoja na madai ya kuhusika kwake katika ghasia za Januari 6, mashtaka ya kuingilia uchaguzi wa 2020 katika jimbo la Georgia, na mashtaka ya kushughulikia vibaya nyaraka za siri zilizopatikana nyumbani kwake.