1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump apigwa marufuku kushiriki uchaguzi Maine

29 Desemba 2023

Jimbo la Maine limempiga marufuku rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kushiriki uchaguzi wa kuwateua wagombea wa urais katika uchaguzi wa mwaka ujao. Maine limekuwa jimbo la pili nchini humo kuchukua uamuzi kama huo.

https://p.dw.com/p/4ahBa
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump Picha: Brandon Bell/Getty Images/AFP

Mkuu wa Uchaguzi katika jimbo hilo la Maine, Shenna Bellow anayetokea chama cha Democrat, amesema Trump wa chama cha Republican ambaye ni mmoja ya wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho, alichochea uasi alipoeneza habari za uwongo kuhusu udanganyifu wa kura katika uchaguzi wa mwaka 2020 na kisha akawahamasisha wafuasi wake kuandamana hadi katika jengo la bunge la Marekani ili kusitisha zoezi la wabunge la kuidhinisha matokeo hayo. 

"Katiba ya Marekani hairuhusu uhalifu katika taasisi za serikali yetu," alisema Bellow katika uamuzi wake alioutoa hapo jana. Hata hivyo, uamuzi huo unaweza kukatiwa rufaa katika mahakama ya juu zaidi na timu ya wanaoendesha kampeni za urais za Trump imesema inapanga kupinga uamuzi huo mahakamani, wakiuita "uamuzi wa kikatili."

Mahakama Colorado imemzuia Donald Trump kuwania urais jimboni humo

Mawakili wa rais huyo wa zamani pia wamekanusha mteja wao kushiriki uasi na kwamba matamshi yake kwa wafuasi wake siku hiyo yalikuwa yanalindwa na haki yake ya uhuru wa kujieleza.

Hatua ya kumpiga marufuku Trump kushiriki uchaguzi imejiri wakati wabunge wa jimbo hilo la Maine walipoiidhinisha wakitumia kifungu cha katiba cha marufuku ya uasi, kinachowapiga marufuku wanasiasa wanaotuhumiwa kuiasi katiba kushika wadhifa wa urais. Kimberley Rosen, Thomas Saviello na  Ethan Strimling walisema katika taarifa yao kwamba uamuzi wa Bellow unasimamia demokrasia na katiba ya nchi.

Uamuzi wa Maine unaweza kumuathiri Trump katika uchaguzi wa Novemba

Jengo la bunge la Marekani mjini Washington
Jengo la bunge la Marekani mjini Washington Picha: Eric Baradat/Getty Images/AFP

Uamuzi huo unalihusu tu jimbo la Maine katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Machi lakini unaweza kuathiri nafasi ya Trump katika uchaguzi mkuu wa Mwezi Novemba. Uamuzi huo pia utaongeza shinikizo kwa Mahakama ya juu ya Marekani kujadili uhalali wa Trump kushiriki katika uchaguzi wa kitaifa chini ya Ibara ya Tatu ya Katiba ya Marekani.

Uamuzi kama huo ulitolewa wiki iliyopita na mahakama ya  Colorado iliyosema kwamba Trump hana sifa ya kushika wadhifa wa rais na kumpiga marufuku pia ya kushiriki uchaguzi wa kuwateua wagombea wa urais katika jimbo hilo.

Trump agoma kurudi mahakamani

Trump ameshitakiwa katika kesi ya taifa na jimbo la Georgia zinazomkabili kufuatia nia yake ya kutaka kubadili matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 lakini bado hajashitakiwa kwa kosa la uasi linalofungamanishwa na jukumu lake la Januari 6 mwaka 2021 katika majengo ya bunge.

Wiki hii Mahakama ya juu katika jimbo la Michigan ilikataa ombi la kumuondoa Trump katika uchaguzi wa mwaka 2024. 

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

afp,reuters