BERLIN : Chama cha Kijani chaunga mkono mradi wa kombora
19 Aprili 2005Chama cha Mazingira nchini Ujerumani inaonekana kuunga mkono kujihusisha kwa nchi hii katika mradi wa kombora la MEADS.
Mwenyekiti mshirika wa chama cha Kijani Reihard Bütikofer ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Berlin kwamba baraza kuu la chama hicho limependekeza kwamba kundi lake la wabunge katika serikali ya mseto lipige kura kuunga mkono mpango huo licha ya mashaka miongoni mwa wanachama wa chama hicho wanaopinga vita.
Kuhusika kwa Ujerumani katika mradi huo kulitumbukia mashakani mwezi uliopita wakati chama hicho cha Kijani kilipohoji mahitaji yake ya kijeshi na gharama.Mfumo huo wa Kujihami wa Kombora la Masafa ya Kati lililoboreshwa kufika mbali zaidi unaojulikana kwa kifupi kama MEADS unakusudia kuhami wanajeshi au maeneo nyeti kutokana na mashambulizi ya anga ya kombora au ndege.
Serikali ya Ujerumani inatazamiwa kugharamia asilimia 25 ya mradi huo wa pamoja kati ya Marekani,Ujerumani na Italia.
Gharama za Ujerumani zimekadiriwa kufikia euro milioni 890 katika kipindi cha miaka minane.
.