ANC yaelekea kupoteza wingi wa kura Afrika Kusini
30 Mei 2024Matokeo ambayo yanaweza kuwa mabadiliko makubwa ya kisiasa tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi.
Kulingana na takwimu za tume ya uchaguzi, kufikia sasa asilimia 11.3 ya kura zimeshahesabiwa, na chama cha ANC kimepata asilimia 42.8 ikifuatiwa na chama cha kileberali cha Democratic Alliance kwa asilimia 26.5 ya kura huku chama cha mwanasiasa Julius Malema cha Economic Freedom Fighters EFF kikichukua nafasi ya tatu kwa asilimia 8.3.
Akizungumza wakati wa zoezi la kuhesabu kura Nombuyiselo Biyela, msimamizi wa kituo kimoja cha kupigia kura katika mji wa Eshowe, jimbo la KwaZulu Natal, amesema;
Kwa kweli hatuwezi kusema itachukua muda gani lakini kwa makadirio yetu, haipaswi kuchukua muda mrefu sana kwa sababu tulihifadhi rekodi za takwimu zetu siku nzima. Sasa ni jukumu letu kuona jinsi mchakato unavyokwenda kwa sababu hatujui kama tuna kura zilizoharibika au la. Kwa hivyo, itabidi tusubiri na tuone itachukua muda gani."
Soma pia: ANC yamsimamisha uanachama Zuma baada ya kuunga mkono chama kipya
Ikiwa matokeo ya mwisho yatafuata takwimu za awali, ANC italazimika kufanya makubaliano na chama kimoja au zaidi kuunda serikali ya mseto, hali ambayo inaweza kuongeza joto la kisiasa katika wiki au miezi kadhaa ijayo nchini Afrika Kusini.
Mazingira magumu kwa ANC
Huku ANC bado ikisalia kuwa chama kikubwa zaidi, kiongozi wake Cyril Ramaphosa huenda akasalia kuwa rais wa nchi hiyo, ingawa matokeo duni yanaweza kumfanya awe katika mazingira magumu na kukabiliwa na changamoto ya uongozi ndani ya chama chake.
Kwa mujibu wa sheria, tume ya uchaguzi ina siku saba kutangaza matokeo kamili, lakini kwa kawaida zoezi hilo hukamilika kabla ya muda ulioratibiwa. Kwa mfano katika uchaguzi uliopita, mnamo 2019, upigaji kura ulifanyika Jumatano
na matokeo ya mwisho yalikuja Jumamosi.
Bunge jipya lazima likutane ndani ya siku 14 baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa na jukumu lake la kwanza ni kumchagua rais.
ANC imekuwa ikishinda uchaguzi wa kitaifa unaofanyika kila baada ya miaka mitano tangu uchaguzi mkuu wa 1994, ulioashiria mwisho wa ubaguzi wa rangi ambapo Nelson Mandela alichaguliwa kuwa rais.
Lakini tangu wakati huo uungwaji mkono wa ANC umepungua kutokana na raia kukatishwa tamaa na masuala kama vile ukosefu mkubwa wa ajira, uhalifu, kukatika kwa umeme mara kwa mara na rushwa.
Katika jimbo la KwaZulu-Natal, mkoa wa mashariki wenye watu wengi, chama kipya kinachoongozwa na rais wa zamani Jacob Zuma, Mkhonto we Sizwe (MK), kimejizolea asilimia 42.3 ya kura dhidi ya 20.1 kwa ANC.
Zuma alilazimika kujiuzulu kama rais mwaka wa 2018 baada ya mfululizo wa kashfa na tangu wakati huo ametofautiana na uongozi wa ANC.