ANC yamsimamisha uanachama Jacob Zuma
30 Januari 2024Uamuzi huo ambao ulitarajiwa na wengi, unatizamwa kama ishara nyingine ya mgawanyiko ndani ya chama hicho kikongwekuelekea uchaguzi wa mwaka huu, ambao huenda ukashuhudia chama cha ANC kilichotawala kwa muda mrefu kikipoteza ushawishi.
Katibu Mkuu wa ANC, Fikile Mbalula alisema kuwa Zuma, atachunguzwa na kamati ya nidhamu na chama kitachukua hatua za kisheria dhidi ya chama kipya ambacho kinafanya kampeni kwa kutumia jina lake. Fikile amewaeleza waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba "Zuma na wenzake ambao matendo yao yanakinzana na maadili na kanuni zétu, watajikuta nje ya chama cha ANC".
Zuma ambaye amekuwa rais wa nne wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 2009 hadi 2018 aliondolewa madarakani baada ya kugubikwa na wimbi la kashfa za ufisadi na tangu wakati huo amejitenga na chama hicho alichowahi kukiongoza. Mnamo mwezi Desemba, Zuma alitangaza kwamba atakiunga mkono chama kipya cha uMkhonto We Sizwe kwa kifupi MK, kikimaanisha Mkuki wa Taifa.
Mgawanyiko ndani ya ANC: Chama cha ANC chagawanyika katika makundi yanayomuunga mkono na yanayompinga Ramaphosa
Jina hilo linatokana na tawi la zamani la kijeshi la ANC wakati wa mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi. Kulingana na Fikile ANC inakusudia kupeleka malalamiko katika mahakama ya uchaguzi ili chama hicho kifutiwe usajili na kupinga matumizi ya jina la MK.
"Kuundwa kwa Chama cha MK si kwa bahati mbaya. Ni jaribio la makusudi la kutumia historia ya kujivunia ya mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa kibaguzi ili kupata uaminifu kwa kile ambacho ni ajenda ya kupinga mapinduzi," alisema Fikile.
Licha ya tangazo lake la kuunga mkono chama cha MK, Zuma hakujiondoa ndani ya ANC na kusababisha baadhi ya wachambuzi kusema kwamba alitarajia kufukuzwa ndani ya chama ili kupata uungwaji mkono zaidi. Tangu wakati huo amekuwa mwiba kwa chama cha ANC, ambacho kimekuwa madarakani kwa miongo mitatu nchini Afrika Kusini.
Kura za maoni zinaashiria kwamba kuondoka kwa Zuma ndani ya ANC kunaweza kusababisha chama hicho kupoteza wapiga kura wengi.
Soma : Zuma aanza kutumikia kifungo cha miezi 15 jela
Mapema mwezi huu, utafiti wa kura za maoni ulionyesha kwamba raia mmoja kati ya watatu wa Afrika Kusini anamuunga mkono mwanasiasa huyo, haswa katika jimbo lake la nyumbani la KwaZulu-Natal ambako kumekuwa uwanja muhimu wa mapambano ya uchaguzi.
Zaidi ya watu 300 walikufa katika ghasia za mwaka 2021 wakati mwanasiasa huyo alipopelekwa jela kwa kudharau mahakamabaada ya kukataa kutoa ushahidi katika kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimkabili wakati akiwa rais.
Wachambuzi wanasema ANC inakabiliwa na kibarua kizito katika uchaguzi wa mwaka huu, katikati mwa ongezeko kubwa la umaskini na ukosefu wa ajira.