Al-shabaab yashambulia kambi ya walinda amani wa AU
3 Mei 2022
Mubarak Mohamed, afisa mkuu wa kijeshi nchini Somalia, ameliambia shirika la habari la Ujerumanui dpa leo Jumanne kwamba mlipuaji wa kujitoa muhanga alitumia bomu lililotegwa ndani ya gari na kuingia katika kambi ya jeshi iliopo katika kijiji cha Elbaraf kilichopo katika mkoa wa Shebelle, na kuzusha mapigano makali yaliosababisha makumi ya wanajeshi wa Burundi kuuwawa waliokuwa kambini hapo huku idadi ya majeruhi haijajulikana.
Baadhi ya wakaazi ambao wanaishi karibu na kijiji hicho kilicho umbali wa kilometa 130 kutoka kaskazini mwa mji mkuu Mogadishu.
Walisema waliamshwa na milipuko mikubwa asubuhi na mapema,ikitokea katika kambi ya walinda amani wa Umoja wa Afrika na baadae kufuatiwa na mabishano makali ya milio ya risasi, kati ya wanapiganaji hao na askari kutoka katika kambi hiyo yaliodumu kwa takriban saa moja.
Soma zaidi:Viongozi wa Somalia wavutana juu ya kumfukuzwa mjumbe wa Umoja wa Afrika
Moshi mwingi kutoka katika kambi hiyo ulitanda hewani wakati wa mapigano hayo makali, ambao uliwalazimu baadhi ya wakaazi kuukimbia mji huo.
Helikopta za walinzi wa amani wa Umoja huo zilitumika kusaidia wanajeshi wa Burundi ambao wanadumisha udhibiti wa eneo hilo.
Al-shabaab yakiri kuhusika na shambulio
Al-shabaab, ambayo imekuwa ikitekeleza mashambulizi dhidi ya serikali kuu ya Somalia kwa zaidi ya muongo mmoja, imetoa taarifa kupitia kituo chake cha redio kinachotumika kuendesha propaganda zake na kudai kuhusika na shambulio hilo baya.
Wapiganaji hao wamesema wamechukua udhibiti wa kambi hiyo na kuua wanajeshi 59 wa Umoja wa Afrika na kujeruhi makumi wengine.
Madai hayo hayakuweza kuthibitishwa mara moja kutoka upande wa serikali ya Somalia wala walinda amani kutoka Umoja wa Afrika.
Mnamo Septemba 2015,takriban wanajeshi 50 wa Umoja wa Afrika waliliripotiwa kuuwawa wakati wapiganaji wa Al-shabaab walipovamia kambi ya kijeshi huko Janale, kusini magharibi mwa Mogadishu.
Soma zaidi:Shambulio la Al-Shabaab laua watu kadhaa Mogadishu
Oktoba 2011 wapiganaji wao walidai kuuwa askari 70 wa Burundi ambao walikuwa kwenye ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Afrika katika vita.
Kwa wakati huo Umoja wa Afrika ulisema umepoteza takriban wanajeshi 10, na kutupilia mbali madai ya wanamgambo hao.
Ujumbe huo mpya wa kulinda amani uliochukua hatamu baada ya kikosi cha awali cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa AMISOM kumaliza muda wake mwezi Machi, kinajukumu la kusaidia vikosi vya Somalia kulinda usalama katika taifa hilo la Pembe ya Afrika lenye matatizo chungumzima.