1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga aua watu watano Mogadishu

Zainab Aziz Mhariri: Yusra Buwayhid
2 Januari 2021

Watu wasiopungua watano wameuawa Jumamosi kwenye shambulio la kujitoa mhanga mjini Mogadishu. Mamlaka ya Somalia imesema mshamuliaji huyo aliwalenga raia wa Uturuki wanaoishi nchini humo.

https://p.dw.com/p/3nSRk
Somalia Mogadischu Autobombe an Checkpoint
Picha: Reuters/F. Omar

Waziri wa Afya wa Uturuki Fahrettin Koca amesema raia wawili wa Uturuki waliuawa katika shambulio hilo na wengine watatu ni miongoni mwa watu 14 waliojeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali ya mjini Mogadishu iliyopewa jina la rais wa Uturuki.

Afisa mwandamizi wa polisi wa Somalia Ali Hassan amesema mshambuliaji huyo aliyejitoa mhanga, ni miongoni mwa watu waliofariki.

Soma zaidi:Jeshi la Somalia lawauwa al-Shabba 16, kuwakomboa watoto 40

Wizara ya mambo ya ndani ya Siomalia imelaani vikali shambulio hilo baya lililowalenga wafanyikazi wa kampuni ya Uturuki inayojenga barabara ya ambayo ilichukua barabara ya Mogadishu-Afgoye ambayo ujenzi wake utachangia maendeleo na ustawi wa Somalia.

Mlipuko huo ulitokea katika eneo la ujenzi lilipo kando ya barabara kati ya Mogadishu na Afgoye, kaskazini magharibi mwa mji mkuu. Wahandisi raia wa Uturuki pamoja na wafanyakazi wa ujenzi walikuwa wakifanya kazi kwenye mradi wa ujenzi wa barabara.

Polisi imesema kundi la kigaidi la al-Shabaab limedai kuwa limehusika na shamulio hilo. Vyanzo vya usalama vya Uturuki vimesema mshambuliaji wa kujitoa muhanga alitumia pikipiki na kwamba shambulio hilo limetokea kilomita 15 mbali na kambi ya jeshi la Uturuki. Kambi hiyo ya jeshi la Uturuki ndio kubwa kabisa iliyopo nje ya nchi iliyofunguliwa mnamo mwaka 2017.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.Picha: Turkish Presidency/AP Photo/picture alliance

Katika miaka ya hivi karibuni Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekuwa mshirika wa karibu wa serikali ya Somalia. Uturuki imejenga shule, hospitali, miundombinu na inatoa udhamini kwa wanafunzi wa Kisomali kwenda kusoma Uturuki.

Uturuki inatoa msaada wa vifaa na mafunzo kwa jeshi la Somalia pia imekuwa inatoa msaada mkubwa kwa Somalia tangu maafa ya njaa kuzuka nchini humo mnamo mwaka 2011. Uturuki inataka kuongeza ushawishi wake katika nchi za Pembe ya Afrika na inakabiliana na wapinzani wake wa nchi za Ghuba kama Saudi Arabia na Falme za Kiarabu.

Soma zaidi:Watu wanane wauwawa katika makabiliano ya risasi Mogadishu

Al-Shabaab, kundi la wapiganaji wenye itikadi kali wanaichukulia Uturuki kuwa mvamizi wa taifa la Afrika Mashariki.

Shambulio hilo la Jumamosi lilitokea saa kadhaa baada ya msemaji wa serikali ya Somalia Ismael Mukhtar Omar kutangaza juu ya shambulio la angani dhidi ya kituo cha radio cha  al-Shabaab katika kijiji cha Kuunyabarow, kusini mwa mkoa wa Shabelle. Msemaji huyo hakueleza ikiwa serikali ya Somalia ilifanya shambulio hilo la angani pamoja na washirika wake wa Marekani.

Umefanyika uharibifu lakini hakuna taarifa za mtu aliyeuawa au kujeruhiwa. 

Vyanzo: RTRE/AP/DPA