1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shaabab yatishia kuishambulia Kenya

14 Januari 2022

Al-Shabaab imetishia katika video mpya kwa kusema "wataianza safari" na kuongeza mashambulizi yake nchini Kenya ili kulipiza kisasi uwepo wa jeshi la nchi hiyo nchini Somalia, ambako kundi hilo lina makao yake. 

https://p.dw.com/p/45Wkp
Dürre Hungersnot Afrika Flash-Galerie
Picha: picture alliance/dpa

Kitengo cha habari cha al-Shabaab kimesema kwenye video hiyo iliyosambazwa kwenye  mitandao ya kijamii ya Rocket Chat na Telegram,

"Tunatuma salamu kwa Kenya, nchi ya makafiri. Tumefunga safari ambayo haina kurudi nyuma. Kwa makafiri, hizi ni nyakati za mwisho."

Chombo cha habari kinachohusishwa na kundi hilo kimedai hivi majuzi kwamba wanamgambo hao walizidisha mashambulizi yao nchini Kenya katika wiki za hivi karibuni kuelekea mwaka mpya.

Soma pia: Watu wanane wauwawa katika makabiliano ya risasi Mogadishu

Tangu Januari 3 mwaka huu, takriban watu 13 wameuawa katika mashambulizi yanayoshukiwa kutendwa na al-Shabab katika mikoa ya pwani ya Kenya iliyo jirani na Somalia.  Al-Shabaab imekuwa ikifanya mashambulizi nchini Kenya tangu mwaka 2011, wakati wanajeshi wa nchi hiyo walipovuka mpaka na kuingia Somalia kupambana na kundi hilo la kigaidi.

Al-Shabaab wanadaiwa kuhusika na mauaji ya raia kaunti ya Lamu

Ijumaa iliyopita, maafisa wanne wa polisi walishambuliwa na kuuawa katika eneo la pwani ya Kenya linalopakana na Somalia ambalo huwa rahisi kuvamiwa na wanamgambo wa Al-Shabaab.

Shambulizi hilo lilitokea katika Kaunti ya Lamu, ambapo serikali ilituma vikosi vya usalama na kutangaza amri ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri baada ya mauaji ya raia saba katika msururu wa uvamizi.

Soma pia: Shambulio la Al-Shabaab laua watu kadhaa Mogadishu

Mapema wiki iliyopita polisi nchini Kenya walishuku kuwa wapiganaji wa Al-Shabaab walihusika na mauaji ya raia saba huko Lamu.

Mtu mmoja alikatwa kichwa na wengine kupigwa risasi au kuchomwa moto hadi kufa katika mashambulio mawili ya Jumapili na Jumatatu. Lakini polisi baadaye walisema ghasia hizo zilihusishwa na mzozo wa ardhi katika eneo hilo.

Wizara ya mambo ya ndani ya Kenya ilitangaza Jumatano iliyopita kuwa baadhi ya sehemu za kaunti ya Lamu ni "maeneo yenye misukosuko" na kusema timu ya usalama itakayowajumuisha mawakala mbalimbali itafanya msako wa kutafuta silaha katika eneo hilo.