1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma apewa saa 48 kujiuzulu

13 Februari 2018

Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC kimekubaliana kumuondoa rais Jacob Zuma kama kiongozi wa taifa hilo, vyombo mbalimbali vya habari vya nchini Afrika Kusini vimeripoti.

https://p.dw.com/p/2sZiN
Südafrika Jacob Zuma
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/A. Ufumeli

MM T/ J2.13.02.2018-Südafrika- Stimmung - MP3-Stereo

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC kimekubaliana kumuondoa rais Jacob Zuma kama kiongozi wa taifa hilo, baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari vya nchini Afrika Kusini vimeripoti. Hatua hiyo inafuatia kikao kilichochukua masaa 13, kilichojumuisha maafisa wa juu wa chama. Taarifa hii ni kulingana na vyombo mbalimbali vya habari. 

Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na chanzo kutoka ndani ya chama hicho zinasema kwamba, katibu mkuu wa ANC amekwenda kuonana na rais Jacob Zuma ili kumuarifu kuhusu uamuzi huo wa chama wa kumuondoa kwenye mamlaka hayo.

Taarifa za mapema hii leo kutoka ndani ya kamati kuu ya chama hicho yenye wajumbe 107, iliyokutana kwa masaa 13 kuanzia siku ya Jumatatu hadi hii leo kujadili kuhusu mustakabali wa Zuma, zilisema Zuma amepewa masaa 48 ya kujiuzulu, baada ya wiki moja ya minong’ono kuhusu hatma ya kiongozi huyo.

Gazeti la Times limeripoti kwamba kulingana na vyanzo kadhaa, kikao hicho cha masaa 13 kilikuwa ni kigumu hadi kufikiwa kwa maamuzi hayo ya kumuondoa Zuma madarakani, huku vyombo vingine vya habari vikarifu kwamba chama hicho kitamuandikia barua Zuma kumtaka kujiuzulu kama rais wa taifa hilo kubwa kiuchumi barani Afrika, baada ya kuomba kuendelea kusalia mamlakani kwa miezi mingine kadhaa.

Mapema, shirika la habari la serikali nchini humo SABC liliarifu kwamba ANC imempa Zuma masaa 48 ya kung'oka madarakani.  Hata hivyo hakujatolewa taarifa rasmi na maafisa wa ANC hawakupatikana kuthibitisha taarifa hiyo. Hata hivyo, taarifa zilizotolewa baadae zilisema ANC kitafanya mkutano na waandashi wa habari majira ya saa nane mchana hii leo kuzungumzia matokeo ya kikao hicho na mustakabali wa Zuma. 

Südafrika, Protest gegen den Präsidenten Jacob Zuma
Rais Zuma amekuwa akikabiliwa na shinikizo kutoka ndani ya chama chake la kumtaka kujiuzuluPicha: picture-alliance/T.Hadebe

Zuma atakabiliwa na kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye iwapo atagoma kung'oka.

Kamati hiyo kuu ya chama ina uwezo wa kumtaka kiongozi wa nchi kuachia madaraka, kimsingi kumlazimisha kujiuzulu, lakini hawajibiki kwa namna yoyote kikatiba kuheshimu hatua hiyo. Hivyo basi, anaweza kukabiliwa na kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye ndani ya siku kadhaa.

Makamu wa rais, Cyril Ramaphosa aliripotiwa kuondoka kwenye kikao hicho ambacho kiliendelea hadi usiku wa manane, ili kukutana na Zuma kwenye makazi yake rasmi yaliyoko Pretoria. Msafara wake ulionekana kurejea kwenye ukumbi kulipokuwa kunafanyika kikao hicho usiku wa manane, na masaa matatu baada ya kurejea kikao hicho kikafungwa. 

Ramaphosa, kiongozi asiyepingwa na anayetarajiwa kuwa rais wa taifa hilo, amekuwa akifanya mazungumzo na Zuma ambaye alikataa ombi la awali kutoka kwa viongozi wa chama chake la kumtaka ajiuzulu, zaidi ya wiki moja iliyopita.

Mkwamo uliohusiana na mustakabali wa Zuma uliitumbukiza Afrika Kusini katika hali ya sintofahamu kuhusu nani anayeiongoza nchi, wakati ambapo shughuli nyingi za umma zilifutwa, ikiwa ni pamoja na hotuba ya mwaka ya hali ya taifa iliyotarajiwa kutolewa Alhamisi iliyopita mbele ya bunge.  

Tangu Ramaphosa alipochaguliwa kuwa kiongozi wa ANC Disemba mwaka jana, Zuma amekabiliwa na ongezeko la miito ya kumtaka ajiuzulu kutoka ndani ya chama chake.

Zuma mwenye miaka 75 amekuwa rais mtata zaidi wa Afrika Kusini tangu kumalizika kwa utawala wa wachache mwaka 1994 nchini humo, na taifa hilo limeshuhudia miaka 9 ya kuporomoka kwa uchumi na mlolongo wa madai ya rushwa.

Mwandishi: Lilian Mtono/dw/afpe/rtre
Mhariri: Grace Patricia Kabogo