Zoezi la upandaji miti Kenya lan'goa nanga
13 Novemba 2023Akiongoza wakenya, Rais William Ruto aliyesindikizwa na naibu wake na Wake zao, alizindua mpango wa kupanda miti bilioni 15 katika kaunti ya Makueni. Wakiwa eneo la kinamasi la Kiu, Rais William Ruto alibainisha kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuyanusuru mazingira.
Mawaziri wengine nao pia waliongoza shughuli za kupanda miti kwenye kaunti zote 47. Uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo ya kupanda miti umefanyika eneo la kinamasi la Kiu lililoko Makueni. Miche isiyopungua alfu kumi imenuiwa kupanda leo kwenye maeneo maalum ya kuzindua mpango huo.
Kwa upande wake, waziri wa Mazingira, Misitu na mabadiliko ya tabia nchi Soipan Tuya alifafanua kuwa misitu ndiyo mapafu ya dunia na upo umuhimu wa kuilinda.
Kampeni hii ni sehemu ya mpango wa serikali kuu kuiongeza idadi ya miti kutokea 7.4% hadi 10% kama inavyofafanua katiba ya Kenya. Ifahamike kuwa wakejya walitengewa siku hii mahsusi kupanda miti.
Kenya inapania kuliongeza eneo lililo na misitu kufikia ekari milioni 10.6
Serikali inapania kuliongeza eneo lililo na misitu kufikia ekari milioni 10.6 kupitia mpango wa Taifa wa kupanda miti bilioni 15. Kulingana na wizara ya mazingira, Kenya imegawanywa Katika maeneo 11 kwa kuzingatia mahitaji ya kiekolojia ili kupanda miti mahsusi kwa kila sehemu. Lorraine Kabaka ni mtaalam wa mazingira na tabia nchi na kwa mtazamo wake kila sehemu inahitaji mbinu maalum.
Ili kuimarisha ufuatiliaji wa miche iliyopandwa, idara ya misitu imezindua app maalum ya Jaza Miti itakayowawezesha kujua idadi iliyopandwa na inavyokua. Zoezi hili linafanyika wakati wa msimu wa Vuli ambao umegubikwa na hali ya El Niño inayosababisha mafuriko.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya