Zelensky azuru mji wa Bucha nje ya jiji la Kyiv
4 Aprili 2022Uingereza imelaani mauaji ya raia nchini Ukraine, iliyoyataja kuwa kuwa ya kishenzi, ingawa imejizuwia kuyaita mauaji ya kimbari.
Msemaji wa Waziri Mkuu Boris Johnson, Max Blain, anasema miili iliyopatikana kwenye maeneo yaliyochukuliwa na wanajeshi wa Ukraine baada ya wale wa Urusi kuondoka ilionyesha mashambulizi ya dharau dhidi ya raia wasio na hatia, na ni ushahidi zaidi kwamba Putin na jeshi lake wanafanya kile kinachoonekana kuwa uhalifu wa kivita nchini Ukraine.
Akiwa kwenye mji wa Bucha muda mufupi uliopita, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anasema mauaji ya Bucha yatachukuliwa kuwa mauaji ya kimbari.
''Huu ni uhalifu wa kivita, na utatambuliwa na ulimwengu kama mauaji ya halaiki. Mko hapa na mnaweza kuona kilichotokea. Tunajua kwamba maelfu ya watu waliuawa na kuteswa, kuvunjwa viungo, wanawake kubakwa na watoto kuuliwa."
Soma pia→'Mauaji ya kimbari ya Bucha' yaiweka pabaya zaidi Urusi
Marekani yataka urusi iondolewe kwenye tume ya haki za binadamu
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet amesema katika taarifa Jumatatu kwamba ameshtushwa na picha za raia ambao wamelala wakiwa wamekufa barabarani na makaburi ya pamoja. Ameongeza kuwa ripoti zinazojitokeza kutoka eneo hilo na maeneo mengine huongeza maswali mazito na ya kutatiza juu ya uwezekano ya uhalifu wa kivita.
Bachelet amesema ni muhimu kwamba miili yote ifukuliwe na kutambuliwa na hatua zote zinapaswa kuchukuliwa kuhifadhi ushahidi.
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield amesema leo kwamba Marekani inapanga kuwasilisha azimio la kusimamishwa kwa Urusi kama mwanachama wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa. Huku Moscow yenyewe ikisema mauaji hayo ni ya kubuni ili kulichafuwa jina lake kwa makusudi.
Juhudi za kidiplomasia za nchi za Kiarabu
Ufaransa, Uingereza, Marekani, Ujerumani na Poland zimetaka vikwazo vikali zaidi vichukuliwe dhidi ya Urusi, ingawa hadi sasa hakujawa na msimamo wa pamoja wa jinsi ya kuchukuwa hatua hizo, huku kila nchi ikitumia njia zake.
Huku hayo yakijiri, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi tano za Kiarabu wamesafiri hadi Moscow kwa ajili ya mazungumzo kuhusu vita nchini Ukraine. Mawaziri Misri, Algeria, Iraq, Jordan na Sudan watakutana baadae leo na waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov.