1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Mauaji ya kimbari ya Bucha' yaiweka pabaya zaidi Urusi

4 Aprili 2022

Ushahidi wa miili iliyopigwa risasi kwa karibu na kaburi la pamoja lililogunduliwa kwenye maeneo yaliyochukuliwa na wanajeshi wa Ukraine baada ya wale wa Urusi kuondoka unazidi kuiweka pabaya Urusi inayokanusha kuhusika.

https://p.dw.com/p/49QT7
Ukraine | Leiche mit gefesselten Händen in Bucha
Picha: Vadim Ghirda/AP/picture alliance

Taras Shapravskyi, naibu meya wa mji wa Bucha, ulio umbali wa kilomita 20 kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Kyiv, alisema siku ya Jumatatu (4 Aprili) kwamba miili 50 kati ya 300 iliyoonekana baada ya wanajeshi wa Urusi kuondoka kwenye mji huo wiki iliyopita, ilikuwa ya watu waliouawa kwa makusudi na vikosi vya Urusi.

Ukraine yailaumu Urusi kwa uhalifu wa kivita huku mji wake Odessa ukikabiliwa na mashambulizi ya anga.

Waandishi wa habari wa shirika la Reuters waliiona maiti moja iliyotupwa kando ya barabara, mikono yake ikiwa imefungwa kwa nyuma na ikiwa na tundu la risasi kwenye paji lake la uso, ingawa shirika hilo halikuweza kuthibitisha idadi iliyotajwa na naibu meya huyo wa Bucha wala waliohusika na mauaji hayo.

Mamlaka nchini Ukraine zinasema zinachunguza uwezekano kwamba Urusi imetenda makosa ya uhalifu wa kivita.

Urusi yakanusha

Baadhi ya viongozi wa ulimwengu wameshutumu mauaji ambayo yamefanyika Bucha Ukraine na kuyataja kuwa uhalifu wa kivita.
Baadhi ya viongozi wa ulimwengu wameshutumu mauaji ambayo yamefanyika Bucha Ukraine na kuyataja kuwa uhalifu wa kivita.Picha: Mykhaylo Palinchak/ZUMA Press/dpa/picture alliance

Hata hivyo, Moscow yenyewe inasema picha za mauaji hayo ni za kubuni ili kulichafuwa jina lake kwa makusudi. 

Tayari Urusi imeomba kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu taarifa za mauaji hayo ya maangamizi ya Bucha, inayosema ni uchokozi dhidi yake.

Ukraine yachukua udhibiti wa eneo la Kyiv kutoka kwa Warusi

Lakini Uingereza inayoshikilia urais wa baraza hilo kwa sasa, imesema hakutakuwa na kikao hicho kwa sasa.

Kwa upande mwengine, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kuwa mashambulizi ya jeshi lake la anga yamepiga vituo 14 vya kijeshi nchini Ukraine usiku wa kuamkia Jumatatu, vikiwemo viwili vya kuongozea mapigano na mitambo miwili ya kutunguwa makombora. 

Mashambulizi yaendelea

Msemaji wa wizara hiyo, Igor Konashenkov, aliwaambia waandishi wa habari mjini Moscow kwamba mfumo wa ulinzi wa anga wa Urusi pia ulizidunguwa ndege sita zisizo rubani za Ukraine karibu na miji ya Mykolaiv, Kherson, Kurakhiva, Indunstrialnoe na Velyka Novosilka.

Ukraine imeituhumu Urusi kwa kufanya mauaji ya kikatili dhidi ya raia katika mji wa Bucha.
Ukraine imeituhumu Urusi kwa kufanya mauaji ya kikatili dhidi ya raia katika mji wa Bucha.Picha: Rodrigo Abd/AP Photo/picture alliance

Miji ya kusini mwa Ukraine yashambuliwa na Urusi

"Kwa ujumla, ndege 125 za Ukraine na helikopta 91, ndege zisizo rubani 392, mifumo 226 ya kukinga makombora ya angani, makombora 833, na pia magari 1,800 ya kikosi maalum cha kijeshi, vifaru 1,936 na magari mengine ya kivita, mifumo 211 ya kufyatulia makombora imeharibiwa tangu kuanza kwa operesheni maalum ya kijeshi." Alisema Konashenkov.

Taarifa kutoka mashariki mwa Ukraine zinasema mashambulizi kwenye mji wa Kharkiv yameuwa watu 50, baada ya makombora kuangukia kwenye mji wa bandari wa Odesa jana Jumapili, ambako Urusi inasema iliharibu ghala la mafuta linalotumiwa na jeshi la Ukraine. 

Uingereza, Marekani, Ujerumani na Poland zimetaka vikwazo vikali zaidi vichukuliwe dhidi ya Urusi, ingawa hadi sasa hakujawa na msimamo wa pamoja wa jinsi ya kuchukuwa hatua hizo, huku kila nchi ikitumia njia zake.