WHO yatangaza Ebola janga la kimataifa
8 Agosti 2014Shirika la afya duniani WHO limeonya kuwa ugonjwa wa Ebola sasa unageuka kuwa janga la kimataifa. Hilo linathibitishwa pia na maafisa wa afya wa Marekani wanaokiri kuwa sasa Ebola imesambaa kuelekea dunia nzima baada ugonjwa huo kulipuka katika nchi za Afrika Magharibi. WHO imeihimiza jumuiya ya kimataifa kutoa misaada ya kifedha na kitaalamu ili kuudhibiti ugonjwa huu unaosambaa kwa kasi.
Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa WHO Dr. Margaret Chan alisema: "Huu ni mlipuko mkubwa zaidi na mgumu zaidi kuwahi kutokea kwa miaka 40. Kamati ya dharura ya WHO imekubaliana kwamba mlipuko wa ugonjwa huu una vigezo vya kuwa dharura ya kimataifa ya afya ya umma."
Wasiwasi watanda
Mpaka sasa, zaidi ya watu 900 wamefariki kutokana na virusi vya Ebola. Wakati virusi hivi vikiendelea kusambaa, wasiwasi nao unazidi kutanda miongoni mwa watu. Kila kukicha visa vipya vya maambukizi na vifo vinatangazwa. Kama vile nchini Uganda ambapo maafisa wa afya wanaripoti kuwa mtu mmoja anashukiwa kuwa ameambukizwa virusi hivyo. Mtu huyo alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Entebbe baada ya kuwasili na ndege iliykuwa ikitokea Sudan Kusini. Msemaji wa wizara ya afya ya Uganda anaeleza kuwa mtu huyo alionyesha dalili za homa. Amefanyiwa uchunguzi, matokeo bado yanasubiriwa.
Wakati huo huo wasiwasi unatanda pia katika nchi za Afrika Magharibi ambapo visa vya kwanza vya Ebola viliripotiwa. Liberia, Guinea na Sierra Leone zimetangaza hali ya dharura.
Liberia kuongeza mikakati
Nchini Liberia maaskari wameweka vizuizi vya barabarani kudhibiti idadi ya watu wanaoingia mji mkuu Monrovia. Ni hali inayowaghadhabisha wakaazi. "Kwa sasa hatuwezi hata kuvuka barabara kwenda kuchota maji pale mbele. Tangu jana baadhi yetu hatuna maji ya kunywa wala maji ya kuoga," anaeleza mwanamke mmoja.
Hali mjini Monrovia inazidi kudorora. Kuna ripoti zisemazo maiti za waliokufa kwa Ebola zimezagaa barabarani. Rais wa Liberia amesisitiza kuwa nchi yake itafanya kile iwezekanalo kuudhibiti ugonjwa huu. Lakini bado mapambano dhidi ya Ebola ni changamoto kwa taasisi nyingi za afya kwani virusi vya Ebola husambaa haraka na mpaka sasa hakuna tiba ya ugonjwa huo.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Afp/dpa
Mhariri: Saumu Yusuf