Ebola kuendelea kusababisha maafa zaidi magharibi mwa Afrika
4 Julai 2014Ugonjwa huo unaoenea kwa kasi kwa kuambukizwa na kirusi kinachopatikana katika ukanda wa nchi za joto hadi sasa umeshawaathiri mamia ya watu katika nchi za Guinea, Liberia, na Sierra Leone ambako kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za WHO, idadi ya watu waliopoteza maisha ambao wamethibitishwa au kuhisiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo inafikia 467, na wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo unaweza ukaenea katika ukanda wote wa magharibi mwa Afrika.
Akifunga mkutano huo uliofanyika mjini Accra, Ghana, na kuwashirikisha mawaziri wa afya kutoka nchi za Afrika Magharibi, mkurugenzi msaidizi wa usalama wa afya wa WHO, Keiji Fukuda, amesema kwa sasa ni vigumu sana kutoa jibu la wazi ni jinsi gani ugonjwa unaweza ukaenea au ni lini utatokomezwa.
MSF yatoa tahadhari
"Nina matumaini sote tutaona kuona mabadiliko ya kupungua kwa matukio katika wiki kadhaa zijazo" alisema Fukuda wakati wa mkutano huo.
Marie-Christine Ferir ambaye ni daktari kutoka shirika la madaktari wasio na mipaka(MSF) anasema mlipuko wa ugonjwa huo utaendelea kwa wiki kadhaa na pengine miezi katika baadhi ya maeneo.
Naye Waziri wa Afya wa Liberia Bernice Dahn anaamini kwa namna moja au nyingine mkutano huo wa Accra utawasaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola
Mawaziri wa afya wakutana kuhusu Ebola
Abdulsalami Nasidi anayetokea katika kituo cha kukabiliana na ugonjwa wa ebola nchini Nigeria anasema wamekubaliana kwa pamoja kutoa elimu kwa viongozi wa vijiji juu ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kusaidiana na madaktari ambao wapo katika maeneo yao.
Kutokana na kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo wa Ebola katika baadhi ya mataifa ya magharibi mwa Afrika, mawaziri wa afya kutoka nchi 12 walikutana katika mkutano wa siku mbili uliofanyika mjini Accra Ghana kujadili ni kwa jinsi gani wanaweza wakakabiliana na ugonjwa huo.
Aidha mawaziri hao, walitarajiwa kutoa mapendekezo kwa serikali za kanda wanazotokea katika kukabiliana na Ebola pamoja na kuzindua mpango wa kupiga vita ugonjwa huo ambao unagharimu dola millioni 10 za Marekani.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO, kabla ya mripuko huu wa sasa, ugonjwa wa Ebola umesababisha vifo vya watu wapatao 1,587.
Mwandishi: Anuary Mkama/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef