WHO yaitaja hospitali ya Al Shifa kama "eneo la kifo"
20 Novemba 2023Wito wa shirika la afya duniani WHO unatolewa huku kukiwa na ripoti inayosema kuwa, Israel na kundi la Hamas wamefikia makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano na kuwaachilia huru mamia ya mateka.
Jeshi la Israel la IDF limesambaza video ya kile inachosema ni handaki la wanamgambo wa Hamas chini ya hospitali ya Al Shifa katika ukanda wa Gaza.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, jeshi hilo limeeleza jana Jumapili kuwa walifichua handaki lenye urefu wa mita 55 na kina cha mita 10 chini ya jengo la hospitali ya Al Shifa.
Taarifa ya jeshi la Israel imeendelea kueleza kuwa, vikosi vyake vilipata pia silaha na kugundua mlango mwengine ndani ya handaki hilo, japo hawakutoa taarifa juu ya kilichokuwepo ndani.
Hamas inasisitiza kuendesha mahandaki kadhaa katika ukanda wa Gaza japo imekanusha kumiliki mahandaki chini ya hospitali au sehemu nyengine za raia.