1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO kuanzisha hospitali katika Ukanda wa Gaza

17 Novemba 2023

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema linataka kuweka hospitali katika maeneo ya wazi katika Ukanda wa Gaza, kufuatia uharibifu mkubwa ambao umesababishwa na mashambulizi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4Z2fi
Shirika la afya ulimwenguni
Nembo ya shirika la afya ulimwenguni WHO Picha: Maksym Yemelyanov/Zoonar/picture alliance

Mwakilishi wa WHO katika maeneo yanayokaliwa ya Palestina Richard Peeperkorn amesema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi habari kwa njia ya video.

Hayo yakijiri, jeshi la Israel limesema limepata maiti ya pili ya mmoja wa walioshikwa mateka. Kulingana na jeshi hilo, maiti hiyo imepatikana karibu na hospitali ya Al-Shifa.

Mkuu wa majeshi ya Israel Herzi Halevi ametangaza leo kuwa watatanua operesheni zao katika Ukanda wa Gaza hadi maeneo mengine.

Uhaba wa mafuta wasitisha huduma za kibinaadamu Gaza

Israel ilianzisha operesheni hiyo ya kulipiza kisasi baada ya kundi la wanamgambo la Hams kufanya shambulizi la kushtukiza ndani ya Israel Oktoba 7, na kuua watu wapatao 1,200. Katika operesheni za Israel Gaza, zaidi ya watu 11,000 wameuawa.

Kwa siku ya pili leo, mifumo ya mawasiliano katika Ukanda wa Gaza imeendelea kutofanya kazi kufuatia ukosefu wa nishati ya kuwezesha intaneti na mitandao ya simu.

Hali hiyo imesababisha pia mashirika ya misaada kusitisha shughuli za kusambaza misaada ya kibinadamu kwenye ukanda huo.