WHO: Omicron inasambaa kwa kasi zaidi ya Delta
19 Desemba 2021Kulingana na shirika la WHO bado wanahitajika kukusanya taarifa zaidi ili kupata ufahamu zaidi wa sababu za kirusi hicho cha omicron kusambaa kwa kasi zaidi ya kirusi aina ya Delta. Lakini pia shirika hilo limesema bado kuna taarifa chache kuhusiana na ufanisi wa chanjo dhidi ya corona, na hasa linapokuja suala la aina hiyo mpya ya kirusi.
"Hospitali nchini Uingereza na Afrika Kusini zinazidi kuelemewa na wagonjwa na kutokana na kuongezeka kwa visa vya maambukizi, kuna uwezekano kwamba mifumo mingi ya afya ikaelemewa haraka," limesema shirika hilo.
Wakati shirika la WHO likionya kuhusu kitisho cha omicron, jana Jumamosi, nchini Ujerumani maelfu ya makundi ya watu wanaopinga chanjo pamoja na sera za serikali kuhusu janga la virusi vya corona waliandamana kupinga vizuizi vya kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona katika miji kadhaa mikubwa ikiwa ni pamoja na Hamburg na Düsseldorf.
Polisi ilisema maelfu ya watu waliingia mitaani katika mji wa Hamburg, kaskazini mwa nchi hiyo, na kutembea katika maeneo kadhaa ya katikati ya mji. Takriban watu 8,000 waliandamana baadhi yakiwa na mabango yaliyoandikwa "Hakuna ulazima wa kuchanja" na mengine yakiwa na maneno "msiwaguse watoto wetu".
Soma Zaidi: Mataifa yajipanga kulazimisha chanjo ya corona kwa wote
Nchini Ujerumani kumeanza kutolewa chanjo kwa watoto, baada ya taasisi ya juu ya chanjo kushauri watoto kuchanjwa. Hata hivyo wazazi wanatofautiana kimawazo katika hili.
Katika mji wa Düsseldorf magharibi mwa Ujerumani takriban watu 4,000 waliandamana. Na polisi ilisema takriban watu 3,500 waliandamana katika mji wa Freiburg na wengine katika miji ya Frankfurt, Karlsruhe, Freiburg na Osnabruck, katika jimbo la Lower Saxony.
Soma Zaidi: Viongozi wa Ujerumani waidhinisha vizingiti vipya vya COVID kwa watu ambao hawajachanjwa
Mawaziri wa afya Ujerumani wataka hatua kali dhidi ya wasafiri.
Katika hatua nyingine, mawaziri wa afya wa majimbo ya Ujerumani jana Jumamosi walitoa mwito wa hatua kali zaidi kwa watu wanaoingia nchini humo ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa kirusi cha omicron, waziri wa afya wa serikali ya shirikisho Karl Lauterbach ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA baada ya mkutano na mawaziri hao wa kujadiliana kuhusu janga hilo
Ujerumani imerekodi visa 6,764,188 vya maambukizi na vifo 108,053, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za karibuni zaidi kutoka kwa taasisi ya kudhibiti magonjwa nchini humo ya Robert Koch.
Nchini Uingereza hali ni tete wakati kukiripotiwa ongezeko la maambukizi la karibu asilimia 30 kwa wiki hii, huku meya wa London Sadiq Khan akitangaza mzozo huo kuwa ni kama "tukio kubwa".
Ujerumani inataraji kuanzisha vizuizi vya kujitenga kwa wasafiri kutoka Uingereza kuanzia usiku wa kuamkia Jumatatu (20.12.2021) na pia watatakiwa kuonyesha uthibitisho wa kutokuwa na maambukizi wanapoingia nchini humo, hii ikiwa ni kulingana na taasisi ya Robert Koch.
Na Uholanzi inatarajia kuingia kwenye kizuizi kikali cha kufunga shughuli kuanzia Jumapili hii katika kukabiliana na kitisho cha ongezeko la maambukizi ya omicron, hii ni kulingana na waziri mkuu wa mpito Mark Rutte alipozungumza na waandishi wa habari.
Rutte amesema hatua hiyo haikuweza kuzuika kutokana na kitisho cha wimbi la tano lililosababishwa na kirusi cha omicron. Maduka, mikahawa, shule na maeneo mengine ya umma yatalazimika kufungwa katika kipindi hicho. Ni maduka ya bidhaa muhimu tu kama ya supermarkets na maduka ya dawa ambayo hayataguswa na sheria hiyo.
Mashirika: DW