WHO: Gaza bado inakabiliwa na kitisho cha njaa
3 Mei 2024Muwakilishi wa Shirika la Afya Duniani katika maeneo ya Palestina Rik Peeperkorn amesema kuwa chakula zaidi kimewasili katika Ukanda wa Gaza katika wiki za hivi karibuni, lakini akaonya kwamba kitisho cha njaa bado hakijatoweka.
Peeperkorn ameongeza kwamba ukilinganisha na miezi michache iliyopita, ni wazi kwamba kwa sasa kunapatikana katika masoko ya Gaza, bidhaa muhimu za msingi kama vile ngano na aina mbalimbali za chakula na si tu katika eneo la kusini bali pia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Daktari Mkuu wa WHO huko Gaza, Ahmed Dahir, amesema usambazaji wa chakula bado hafifu na kuongeza kwamba kitisho cha njaa bado kinainyemelea Gaza. WHO imeongeza kwamba uzalishaji wa ndani wa chakula kama vile matunda na mbogamboga pamoja na uvuvi wa samaki katika Ukanda wa Gaza "vimeharibiwa" na vita.
WHO imeripoti kuwa tangu mwezi Machi, zaidi ya watoto 40 walio na umri chini ya miaka mitano na wenye utapiamlo walipelekwa katika hospitali za Ukanda wa Gaza huku wakiwa pia na matatizo mengine ya kiafya. Baadhi ya watoto wenye umri wa miaka miwili, walikuwa na uzito wa karibu kilo 4 tu, kuliko uzito wa wastani wa kilo 10 hadi 14.
Soma pia: UN yaonya juu ya vitendo vya Israel kuzuia misaada kuingizwa Gaza
Shirika hilo limesisitiza kuwa kabla ya kuzuka mapigano huko Gaza mnamo Oktoba 7, hakukuripotiwa kabisa utapiamlo katika eneo hilo. Peeperkorn anasema athari za utapiamlo kwa watoto hao zitashuhudiwa zaidi katika miaka ijayo.
Kulingana na mamlaka ya afya ya Palestina inayodhibitiwa na Hamas, karibu watoto 25 wenye utapiamlo wamekufa huko Gaza katika wiki za hivi karibuni, huku muwakilishi huyo wa WHO akisisitiza kwamba watoto hao hawakufa kutokana na njaa lakini utapiamlo ulichangia kwa kiasi kikubwa.
Umoja wa Mataifa waionya Israel kuhusu kuishambulia Rafah
Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinaadamu limeonya kuwa maisha ya mamia ya maelfu ya watu yatakuwa hatarini ikiwa Israel itashikilia msimamo wake wa kuendesha operesheni ya kijeshi katika mji wa kusini mwa ukanda wa Gaza wa Rafah.
Uturuki ilitangaza kusitisha mahusiano yake ya kibiashara na Israel huku Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan akisema nchi yake kamwe haitofumbia macho matendo ya Israel huko Gaza.
"Hakuna jambo linalokubalika katika kile kinachoendelea kati ya Israel na Palestina. Hadi sasa, Israel imewaua Wapalestina elfu 40 hadi 45 bila huruma. Na, kama Muislamu, ni jambo lisilofikirika kwetu kukaa tu na kutazama hili likitokea. Hatua zozote zinazohitajika kuchukuliwa, tunazichukua."
Soma pia: Erdogan asema Uturuki inaliunga mkono kikamilifu kundi la Hamas
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akikaidi miito ya Jumuiya ya kimataifa ikiwemo ya mshirika wake mkuu Marekani wa kutoushambulia mji huo wa Rafah ambao unawahifadhi Wapalestina zaidi ya milioni moja waliokimbia mapigano katika maeneo mengine katika ukanda huo. Mashambulizi ya leo huko Rafah yamesababisha vifo vya watu saba wakiwemo wanawake na watoto.
(Vyanzo: Mashirika)