UN yaonya juu ya Israel kuzuia misaada kuingizwa Gaza
19 Machi 2024Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ameonya kuhusu hatari ya kutokea baa la njaa huko Gaza na kukemea hatua za Israel za kuweka vizuizi kwenye mpango wa kuwasilisha misaada huko Gaza.
"Kiwango cha vizuizi vya Israel katika uwasilishwaji wa msaada huko Gaza, pamoja na namna inavyoendelea kufanya mashambulizi, inaweza kuchukuliwa sawa na matumizi ya njaa kama silaha ya vita, jambo ambalo ni uhalifu wa kivita. Muda unakwenda. Kila mtu, hasa wale wenye ushawishi, ni lazima waishinikize Israel kuchukua hatua zitakazowezesha uwasilishwaji na usambazaji wa misaada ya kibinadamu inayohitajika ili kutokomeza njaa na kuepusha hatari ya baa la njaa," alisema Turk.
Wakati mashirika ya misaada yakiilaumu Israel kufuatia hatua yake ya kuizingira Gaza, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema serikali yake imechukua hatua za kuhakikisha misaada hiyo inawasili kikamilifu. Mazungumzo ya kutafuta mpango wa usitishwaji mapigano yanaendelea mjini Doha nchini Qatar.