WFP yasema haitochukua jukumu la UNRWA huko Gaza
2 Novemba 2024Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limesema haliwezi kutumika kama mbadala wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya kiutu kwa Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Kati (UNRWA) huko Gaza.
Mkuu wa ofisi ya WFP Martin Frick ya mjini Berlin ameyasema hayo alipozungumza na vyombo vya habari vya Ujerumani.
Frick alisema, UNRWA ndio uti wa mgongo wa utoaji wa misaada ya chakula, ulinzi na matibabu kwa watu wa ukanda Gaza wanokabiliwa na vita.
Soma zaidi. Israel yakosolewa kwa kutaka kulipiga marufuku UNRWA
Siku chache zilizopita Israel ililipiga marufuku shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa Israel yenyewe itachukua jukumu hilo pamoja na mashirika mengine katika kuratibu na kusambaza misaada katika ukanda wa Gaza.
WFP imesema kulipiga marufuku shirika la UNRWA kutahatarisha zaidi maisha ya watu ambao kwa sasa wanajaribu kuishi kwa kutumia rasilimali zao za mwisho.