1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfghanistan

WFP: Mvua imesababisha vifo vya watu 300 Afghanistan

11 Mei 2024

Mafuriko yanayotokana na mvua kubwa isiyo ya kawaida nchini Afghanistan yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 na kuharibu takriban nyumba 1,000.

https://p.dw.com/p/4fkAH
Athari za mvua kubwa Afghanistan.
Mvua zisizo za kawaida zimesababisha maafa makubwa nchini Afghanistan. Picha: Mehrab Ibrahimi/Xinhua/dpa/picture alliance

Haya yamesemwa leo na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP.

Shirika hilo limesema kuwa linasambaza biskuti maalamu za kutuliza njaa kwa walionusurika katika moja ya mafuriko mengi yaliyoikumba nchi hiyo katika wiki chache zilizopita, hasa jimbo la kaskazini la Baghlan, ambalo liliathirika zaidi hapo jana.

Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kuwa katika mkoa jirani wa Takhar,  mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 20.

Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, msemaji mkuu wa serikali ya Taliban Zabihullah Mujahid, amesema kuwa mamia ya watu wameuawa kwenye mafuriko hayo huku idadi kubwa ya watu wakipata majeraha.

Mujahid ameongeza kuwa maeneo yalioathirika zaidi ni mikoa ya Badakhshan, Baghlan, Ghor na Herat. Pia ameongeza kuwa serikali imeagiza kutumika kwa rasilimali zote zilizopo ili kuwaokoa watu, kusafirisha majeruhi na kutafuta miili ya waliokufa.