Waziri wa zamani wa Gambia kupandishwa kizimbani Uswisi
8 Januari 2024Kesi hiyo yenye mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu inamkabili Ousman Sonko ambaye alikuwa waziri tangu mwaka 2006 hadi 2016.
Anatuhumiwa kusimamia mashambulizi ya kupangwa yaliyotekelezwa na vyombo vya usalama vya Gambia kwa lengo la kuwanyamazisha wapinzani wa utawala wa Jammeh.
Soma pia: Adama Barrow aahidi kuweka ukomo wa muhula wa urais Gambia
Anahusishwa pia kufanya mauaji ya kukusudia, kuwatesa watu, kufanya ubakaji na kwa makusudi kuwanyima watu haki zao za msingi.
Iwapo atatiwa hatiani anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Kesi yake inayosikilizwa kwenye mahakama ya makosa ya jinai kwenye mji wa kusini mwa Uswisi wa Bellinzona ilifunguliwa chini ya misingi ya kimataifa ya utoaji haki ambayo inaruhusu taifa la kigeni kuwashtaki na kuwahukumu watu wanaohusishwa na makosa ya kivitia, mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu.