1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Ujerumani aonya kuhusu ushawishi wa Urusi Sahel

4 Machi 2024

Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani, Svenja Schulze ameonya kuwa ugaidi na ushawishi wa Urusi unatishia usalama wa ukanda wa Sahel, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

https://p.dw.com/p/4d8Rk
Urusi Saint Petersberg| Rais Putin na Traore wa und Burkina Faso
Rais wa Urusi akisalimiana na kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso Ibrahim Traore mjini Saint Petersberg.Picha: Alexander Ryumin/dpa/Tass/picture alliance

Burkina Faso itakuwa kituo cha kwanza kati ya viwili vya waziri Schulze, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Muungano wa Sahel ulioanzishwa na Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya ili kuyasaidia mataifa ya Sahel.

Anatazamiwa kuwa waziri wa kwanza wa Ulaya kuizuru nchi hiyo tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Ibrahim Traoré mwaka 2022.

Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Ujerumani, amesema muungano huo kwa sasa umewekeza kiasi cha euro milioni 28 katika ukanda wa Sahel.

Ameiambia DW kuwa Ujerumani na Ulaya zina nia ya kuwepo uhusiano mzuri na wa ujirani mwema na nchi za Afrika Magharibi, na kwamba hilo linaweza kufanikiwa tu kwa kujitolea, pamoja na sera za heshima za kiutendaji.

Deutschland Berlin | Waziri wa ushirikiano wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze
Waziri wa ushirikiano wa maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze.Picha: Ute Grabowsky/photothek/IMAGO

Matokeo ya ugaidi yanaonekana wazi Burkina Faso. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, takribani watu milioni 2 waliyakimbia makaazi yao Machi, 2023.

Takwimu zilizokusanywa na Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wakaazi wa Burkina Faso walikuwa wanaishi chini ya kiwango cha umasikini mwaka 2020, na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF zinaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 3.4 hawapati huduma za afya.

Soma pia:Tishio la ugaidi ni kubwa katika eneo la migogoro la Afrika 

Kwa miaka mingi, Burkina Faso imekuwa ikishambuliwa na makundi ya wapiganaji wenye itakadi kati za Kiislamu, ambayo yanazidi kusogea karibu na mji mkuu, Ouagadougou. Maelfu ya watu waliuawa mwaka jana pekee.

Adama Sawadogo, anayeishi Ouagadougou ameiambia DW kuwa hali ya usalama inapoimarika kutokana na jeshi kuingilia kati, baadhi ya watu wasio na makaazi wamekuwa wakirejea kwenye vijiji vyao.

Kulingana na Sawadogo, wana uhakika kwamba ugaidi utamalizika Burkina Faso.

Kitisho cha kuenea kwa ushawishi wa Urusi

Akiwa Burkina Faso, Schulze pia anapanga kuitembelea miradi yenye lengo la kutoa mafunzo yenye ustadi kwa vyombo vya habari kupambana na taarifa potofu. Kesho jioni, anatarajiwa kuelekea nchi jirani ya Benin, ambayo inatishiwa na kuenea kwa ghasia kwenye mpaka wake.

Waandamanaji Burkina Faso wakiwa na Bendera ya Urusi
Waandamanaji Burkina Faso wakiwa wamebeba bendera ya taifa hilo la ile ya UrusiPicha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Mwishoni mwa Mwezi Januari, Burkina Faso iliungana na Mali na Niger kutangaza uamuzi wa kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, suala ambalo linatarajiwa kuwa ajenda wakati wa ziara ya Schulze.

Soma pia: Je, Ujerumani inapaswa kupanua ushirikiano kanda ya Sahel?

Kama ilivyo kwa majirani Mali na Niger, ambazo pia zinatawaliwa na jeshi kutokana na mapinduzi ya hivi karibuni, Burkina Faso pia inajisogeza karibu zaidi na Urusi.

Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanaushutumu utawala wa kijeshi kwa kukiuka haki za binaadamu. Ilaria Allegrozzi, mtafiti mwandamizi wa shirika la Human Rights Watch katika ukanda wa Sahel, anasema viongozi wa Burkina Faso wanatumia mbinu za kikatili kuwaadhibu na kuwanyamazisha wakosoaji na wapinzani.