Waziri wa mambo ya nje Ukraine awasilisha barua ya kujiuzulu
4 Septemba 2024Ukraine imekumbwa na wimbi la kujiuzulu mawaziri katika serikali ya rais Volodymr Zelensky. Spika wa bunge Ruslan Stefanchuk, amesema waziri wa mambo ya nje Dmytro Kuleba amewasilisha barua yake ya kujiuzulu leo Jumatano.
Hatua ya Kuleba imefuatia kujiuzulu jana waziri anayehusika na usimamizi wa utengenezaji silaha pamoja na mawaziri wa viwanda, mazingira, sheria na naibu waziri mkuu.
Soma pia:Kuleba yuko ziarani Beijing kutafuta amani nchini Ukraine
Hatua hiyo imekuja wakati rais Zelensky akitarajiwa kufanya mabadiliko makubwa ya serikali yake na huku nchi hiyo ikiwa katika kipindi kigumu kwenye vita vyake na Urusi.
Spika wa bunge Stefanchuk amesema ombi la kujiuzulu waziri wa mambo ya nje litajadiliwa na wabunge hivi karibuni baada ya Rais Zelensky kusema kwamba serikali yake inafanya mabadiliko ili kujiimarisha na kupata matokeo inayoyahitaji.
Taarifa pia zimeeleza kwamba Urusi leo imeushambulia mji wa magharibi mwa Ukraine wa Lviv na kuwauwa watu saba.