1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa fedha Kenya akamatwa

22 Julai 2019

Mkuu wa mashtaka ya umma nchini Kenya ametaka waziri wa fedha nchini humo Henry Rotich na maafisa wengine watiwe mbaroni na wafunguliwe mashtaka kufuatia madai ya rushwa katika mradi wa ujenzi wa mabwawa mawili.

https://p.dw.com/p/3MWt1
Kenia Henry Rotich
Picha: Reuters/T. Mukoya

Waziri wa fedha nchini Kenya Henry Rotich amekamatwa. Rotich amekamatwa kufuatia agizo la mkuu wa mashtaka ya umma Noordin Haji alilolitoa mapema leo. Honry Rotich amekamatwa pamoja na katibu mkuu wa wizara ya fedha Kamau Thuge.

Noordin haji, alitoa agizo la kutaka waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich, akamatwe na kufunguliwa mashtaka ya rushwa kuhusu ujenzi wa mabwawa mawili.

Noordin amesema mashtaka dhidi ya Rotich yanatokana na uchunguzi wa polisi uliofanywa kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika mradi wa kujenga bwawa unaofanywa na kampuni ya ujenzi ya Italia ya CMC Di Ravenna.

Hata hivyo, Rotich amekanusha kuhusika na madai hayo na kampuni hiyo pia imeyakanusha madai hayo. Rotich atashtakiwa pamoja na maafisa wengine kadhaa wa serikali, akiwemo katibu mkuu wa wizara ya fedha, Kamau Thugge.

Noordin Haji amewaambia waandishi habari kwamba maafisa hao walikiuka sheria ya matumizi ya fedha za umma.

Mashtaka dhidi ya Rotich huenda yakasababisha mshtuko kwa wanasiasa wa Kenya, ambao wamezoea kupuuza kashfa za ufisadi, ambapo mara nyingi hatua zinazochukuliwa huwa ni ndogo.