1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Waziri Mkuu wa Poland afanya ziara Ufaransa

12 Februari 2024

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema kwamba Ufaransa na Poland ziko kwenye "ukurasa" linapohusika suala la siasa za kikanda na msaada kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4cKJW
Ursula von der Leyen akiwa na Donald Tusk mjini Brussels
Donald Tusk akiwa na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.Picha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Kauli hii imetolewa katika wakati hamkani inaongeza barani Ulaya juu hali ya usalama katika siku za usoni hasa kutokana na uwezekano wa Donald Trump kuchaguliwa tena kuwa rais wa Marekani.

Soma pia: Tusk atarajia kutatuwa mgogoro wa Poland na Ukraine

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Rais Emmanuel Macron, Tusk amesema wanataka watume ishara ya pamoja kwamba wako tayari kwa mshikamano katika hali zote ngumu na kuuimarisha tena ushirikiano wa mataifa matatu ya Ufaransa, Poland na Ujerumani unaofahamika kama "Weimar Triangle".

Jukwaa hilo la ushirikiano la "Weimar Triangle" lililoundwa mwaka 1991 kwenye mji wa Ujerumani wa Weimar kwa dhima ya kushughulikia masuala yote yanayozihusu kwa pamoja nchi hizo tatu.

"Nataka kusisitiza hapa Paris kwa uwazi kabisa kwamba hakuna mbadala wa Umoja wa Ulaya, hakuna njia mbadala ya ushirikiano wa kati ya Ulaya na Marekani , hakuna mbadala wa NATO. Alisema Tusk.

Soma pia: Poland yataka Ukraine ipatiwe makombora ya masafa marefu

Aliongezea kusema "Ulaya lazima iwe bara salama, na hii ina maana kwamba Umoja wa  Ulaya, Ufaransa na Poland lazima ziwe mataifa yenye nguvu, tayari kutetea mipaka na eneo lao."

Kulingana na chanzo cha serikali ya Poland, Ulaya inapaswa kujipanga na kujiimarisha katika sekta ya ulinzi iwapo Trump atashinda urais, Chanzo hicho kiliongeza kuwa Ulaya inahitaji ushirikiano wa haraka katika utenegenezaji wa risasi na kwamba Poland haitozuia tena kile kinachotajwa kama "uhuru wa kimkakati" unaoifaya Ulaya kutotegemea mataifa mengine.

Ushirikiano na mshikamano nyakati zote

Donald Tusk
Waziri mkuu wa Poland Donald Tusk akizungumza na waandishi wa habariPicha: Omar Havana/AP Photo/picture alliance

Uhusiano kati ya Poland na Ujerumani ulikuwa mbaya kwa miaka minane kutokana na misimamo mikali ya utawala wa chama cha wazalendo uliokuwepo nchini Poland.

Warsaw, Paris na Berlin zinaona ushirikiano katika Umoja wa Ulaya juu ya ulinzi na kuongeza msaada wa mataifa 27 kwa Ukraine kuwa muhimu wakati ambapo uungaji mkono wa Marekani kwa Kyiv unayumba.

Soma pia: Umoja wa Ulaya walaani kitisho cha Trump kwa NATO

Tusk amewasili Paris kama sehemu ya ziara fupi, kisha baadaye anasafiri hadi Berlin kutafuta uhusiano wa karibu na mataifa mawili ya Ulaya yenye nguvu wakati vita nchini Ukraine vikiendelea huku Ulaya ikitazama uwezekano wa Donald Trump kurejea madarakani.

Trump aliibua hasira miongoni mwa washirika wake wa Magharibi baada ya kuashiria kwamba Marekani haitowalinda wanachama wa NATO dhidi ya shambulizi la Urusi ikiwa nchi hizo hazitochangia vya kutosha katika bajeti ya ulinzi ya jumuiya hiyo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, ametoa matamshi makali na yasiyo ya kawaida ya kumkosoa Trump, akisema "pendekezo lolote kwamba washirika hawatalindana linadhoofisha usalama, ikiwa ni pamoja na ule wa Marekani".