Waziri mkuu mpya wa mpito ya Haiti alazwa hospitali
9 Juni 2024Waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Haiti, Garry Conille, amelazwa hospitali katika mji mkuu Port-au-Prince. Vyombo vya habari katika taifa hilo la Caribbean vimesema jana jioni kuwa Conille anaugua ugonjwa sugu wa pumu na amekuwa akikabiliwa na matatizo ya kupumua katika siku za karibuni.
Mipango inafanywa ya kumsafirisha waziri mkuu huyo katika hospitali ya ng'ambo. Mwishoni mwa mwezi uliopita, baraza tawala la Haiti lilimchagua Conille, ambaye alihudumu kama waziri mkuu kuanzia Septemba 2011 hadi Mei 2012, kuwa waziri mkuu wa mpito kuliongoza taifa hilo la Caribbean kutoka kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa.
Wakati kukiwa na mzozo mkubwa unaohusisha tofauti za kisiasa, usalama na utoaji huduma, Conille amepewa jukumu la kusafisha njia kwa ajili ya kufanyika uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu mwaka wa 2016. Aliyekuwa Waziri mkuu wa mpito Ariel Henry, ambaye hakurejea nchini akitokea ziara ya kigeni mwishoni mwa Februari mwaka huu kutokana na hali ya usalama nchini Haiti, alijiuzulu Aprili wakati baraza hilo tawala lilikuwa limeundwa.