1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazimbabwe wapiga kura kuchaguwa rais, wabunge

23 Agosti 2023

Raia wa Zimbabwe wanapiga kura hivi leo kwenye uchaguzi mkuu wa urais na bunge baada ya kampeni iliyotawaliwa na ukandamizaji dhidi ya wapinzani, khofu ya wizi wa kura na hasira ya umma dhidi ya mgogoro wa kiuchumi.

https://p.dw.com/p/4VTSc
Parlamentswahlen in Simbabwe
Picha: Siphiwe Sibeko/Reuters

Maelfu ya wananchi wa Zimbabwe walimiminika vituoni tangu mapema alfajiri na wakaanza kupiga kura zao majira ya saa 1:00 asubuhi. 

Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (ZEC), ilisema raia milioni 6.6 walikuwa wamejiandikisha kuwa wapiga kura katika taifa hilo lenye raia wapatao milioni 15.

Vituo vya kura vilitazamiwa kufungwa saa 1:00 magharibi kwa majira ya Zimbabwe na matokeo yalitakiwa yawe yamekamilika kutangazwa ndani ya siku tano tangu kura zipigwe.

Soma zaidi: Nelson Chamisa, kijana anayepambana na Mnangagwa
Wazimbabwe waanza kupiga kura katika uchaguzi mkuu

Kwenye kiunga kikongwe cha Mbare mjini Harare, wapiga kura walianza kujipanga kwenye mistari tangu alfajiri nje ya mahema yanayotumika kama vituo cha kupigia kura. 

Baadhi walionekana wakitumia simu zao za mikononi kama kurunzi kuthibitisha ikiwa majina yao yamo kwenye orodha ya wapigakura iliyobandikwa nje ya vituo hivyo. 

Kura ya matumaini?

Diana Office, mwanamke mwenye umri wa miaka 30, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba aliwasili masaa mawili kabla ya vituo kufunguliwa ili kuepuka msongomano.

"Ni muhimu kwangu kupiga kura," alisema. Alipoulizwa ikiwa ana matumaini ya mambo kubadilika baada ya uchaguzi, alicheka huku akisema hana matumaini hayo isipokuwa yupo kutekeleza haki yake tu. 

Kuelekea uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe

Rais Emmerson Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 80, aliyeingia madarakani kupitia mapinduzi yaliyomuondosha marehemu Robert Mugabe mwaka 2017, anawania kurejea madarakani.

Mpinzani wake mkuu ni Nelson Chamisa, mwenye umri wa miaka 45 na anayeongoza muungano wa vyama vya upinzani uitwao Citizens Coalition for Change, CCC.

Upinzani, ambao tangu zamani una nguvu zaidi kwenye maeneo ya mijini, unatazamia kufaidika na hali ya kutokuridhika wananchi juu ya hali ya uchumi inayojumuisha kupanda kwa gharama za maisha, ukosefu wa ajira na ufukara. 

Nafasi ya Chamisa

Chamisa alipiga kampeni kwa kaulimbiu ya "Zimbabwe kwa kila mmoja" na kuahidi kukabiliana na ufisadi, kuanzisha mageuzi makubwa ya uchumi na kuiondowa nchi hiyo kutoka kwenye hali ya sasa ya kutengwa kimataifa.

Simbabwe Afrika Veranstaltung Opposition
Nelson Chamisa anayeongoza muungano wa upinzani wa CCC alipiga kampeni kwa kaulimbiu ya "Zimbabwe ya kila mmoja".Picha: KB MPOFU/REUTERS

Hata hivyo, katika taifa ambalo lina historia ya muda mrefu ya chaguzi zenye mashaka, watu wachache ndio wanaoamini ikiwa Chamisa ataweza kutangazwa mshindi. 

Soma zaidi: Maelfu wakusanyika kumuunga mkono Chamisa nchini Zimbabwe

Kawaida, chama tawala ZANU-PF hutumia vyombo vya dola kukandamiza upinzani, na ni shida kuona endapo mwanasheria na mchungaji wa kanisa atakiuka viunzi vya dola na kuongoza serikali ijayo.

Muungano wa upinzani anaouongoza unasema wanachama wake wengi walikamatwa na takribani haukupewa kabisa nafasi ya kujitangaza kupitia televisheni ya taifa.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Rodney Kiwa, alitupilia mbali uwezekano wa kukiukwa kwa kanuni za uchaguzi na wizi wa kura, akisema ni "zao la dhana tupu."

Vyanzo: AP, AFP