Watu watatu wafa kufuatia mlipuko wa gesi jijini Nairobi
2 Februari 2024Msemaji wa serikali Isaac Maigua Mwaura amesema mlipuko huo umesababisha moto mkubwa ambao ulisambaa sehemu kubwa. Mwaura ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kuwa moto huo umeharibu magari kadhaa na mali za biashara, ikiwemo vibanda vya biashara na maduka.
Amesema nyumba za makaazi zilizoko katika eneo jirani pia zimeteketea kwa moto. Mlipuko huo ulitokea usiku wa kuamkia leo kwenye eneo la Embakasi kusini mashariki mwa Nairobi.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema zoezi la kutafuta manusura bado linaendelea.
"Bado tunatafuta iwapo kuna miili ambayo imeteketea katika nyumba tofauti na tunawaomba Wakenya kutuombea. Huu ni wakati ambao tunahuzunishwa na tukio kama hili ambalo halijawahi kutokea kabla."
Watu 222 waliojeruhiwa walikimbizwa kwenye hospitali mbalimbali. Awali, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kuwa takribani watu 300 wamejeruhiwa.