1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliokufa kutokana na moto Guinea yafikia 23

22 Desemba 2023

Idadi ya vifo kutokana na mlipuko na moto uliozuka katika kituo cha mafuta kwenye mji mkuu wa Guinea, Conakry imeongezeka hadi watu 23 kutoka 13.

https://p.dw.com/p/4aSwl
Guinea Explosion
Picha: AP Photo/picture alliance

Taarifa ya serikali imesema idadi ya waliojeruhiwa imepanda hadi 241 kutoka 178. Mabaki ya watu 10 bado hayajatambuliwa, na serikali imepokea ripoti za watu kadhaa kutojulikana waliko. Mlipuko huo uliotokea katika kituo kikuu cha mafuta kinachoshughulika ununuzi wa bidhaa za mafuta ulizusha hofu ya uhaba wa mafuta. Serikali ilisema katika taarifa kuwa usambazaji wa petroli unaendelea kote nchini. Hapo jana, vijana waliokuwa wanaandamana walikabiliana na vikosi vya usalama mjini Conakry huku waandamanaji wakidai petroli iendelee kutolewa katika vituo vya mafuta ambavyo vilifungwa baada ya mkasa huo. Kanali Mamady Doumbouya, mkuu wa serikali ya kijeshi aliyechukua madaraka baada ya mapinduzi ya 2021, ametangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kuanzia jana.