Watu wanane wauawa baada ya Urusi kushambulia soko Ukraine
12 Oktoba 2022Kulingana na gavana wa jimbo la Donetsk nchini Ukraine Pavlo Kyrylenko, watu wasiopungua saba wameuawa na wengine wanane kujeruhiwa kufuatia shambulizi dhidi ya soko moja ambalo lilikuwa na watu wengi kwenye mji wa Avdiivka mapema leo.
Hayo yakijiri, Ukraine imekomboa maeneo zaidi yaliyokamatwa awali na Urusi kwenye miji yake ya kusini. Ukraine imesema hayo huku ikipokea mifumo ya ulinzi ya angani kutoka nchi za Magharibi, ikisema italeta "zama mpya” baada ya mashambulizi mengi ya Urusi dhidi yake.
Ukraine imesema maeneo matano iliyokomboa kusini mwa jimbo la Kherson, ni mojawapo ya majimbo Urusi ilisema ilichukua mwisho wa mwezi Septemba.
Kukombolewa kwa maeneo hayo ni pigo kubwa la hivi karibuni dhidi ya Urusi kufuatia uvamizi wake Ukraine.
Kwa siku mbili sasa, Urusi imefyatua mfululizo wa makombora na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 19. Aidha mashambulizi hayo yameharibu vituo vya nishati nchini Ukraine. Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mashambulizi hayo ni ya kulipa kisasi kufuatia mlipuko katika daraja la Crimea.
Ukraine yaapa kukomboa majimbo yote ambayo Urusi imechukua
Mapema Jumatano, shirika la usalama la Urusi FSB lilisema limewakamata washukiwa wanane wanaohusishwa na mlipuko huo.
Aidha shirika hilo lilisema limezuia majaribio mawili ya mashambulizi dhidi ya Urusi yaliyokuwa yakipangwa na Ukraine.
Licha ya maonyo kutoka Urusi, Ukraine imeapa kuirudisha rasi ya Crimea mikononi mwake pamoja na kukomboa majimbo manne ambayo Urusi inasema sasa ni sehemu yake.
Ikulu ya rais Volodymyr Zelensky imetangaza kupitia taarifa zake za kila siku kuwa miongoni mwa maeneo yaliyokombolowa na vikosi vya usalama vya Ukraine ni Pamoja na Novovasylivka, Novogrygorivka, Nova Kamyanka, Tryfonivka na Chervone.
Hata hivyo taarifa hiyo imeongeza kuwa, vikosi vya Urusi vinaendelea kushambulia ngome za Ukraine.
NATO yajadili kuipa Ukraine mifumo zaidi ya ulinzi
Hayo yanajiri mnamo wakati takriban nchi 50 zikiongozwa na Marekani za Jumuiya ya Kujihami ya NATO na zinazoiunga mkono Ukraine, zikikutana na miongoni mwa ajenda kuu ni kuipa Ukraine mifumo zaidi ya ulinzi wa angani dhidi ya mashambulizi ya angani yanayofanywa na Urusi.
Akizungumza kabla ya mkutano huo wa siku mbili wa mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa jumuiya hiyo, katibu mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amesema kuongeza mifumo ya ulinzi kwa Ukraine ndio kipaumbele.
Mkusanyiko huo wa mawaziri kutoka zaidi ya mataifa 50 ni wa kwanza mkubwa wa NATO tangu Urusi ilipoyanyakua majimbo manne ya Ukraine, kutangaza kuongeza wanajeshi na kutoa vitisho vya kutumia silaha za nyuklia.
Jumuiya ya NATO imezitaja hatua za Urusi kuwa uchochezi wa wazi wa vita.
Umeme wa kinu cha Zaporizhzhia wakatika
Katika tukio jingine linalofungamana na mzozo huo, shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia matumizi ya nishati ya atomiki IAEA limesema kinu kikubwa zaidi barani Ulaya cha nishati ya nyuklia kilichoko Zaporizhzhya Ukraine kimekosa umeme kwa mara ya pili ndani ya siku tano, na kwamba hali hiyo inazusha wasiwasi mkubwa.
Mkuu wa shirika hilo Rafael Grossi ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba hali hiyo kwenye kinu hicho ambacho kipo chini ya udhibiti wa Urusi, inatilia uzito umuhimu wa kuwa na eneo maalum la usalama na kujikinga karibu na kinu hicho.
Kulingana na IAEA, kinu hicho kina mafuta ya kutosha kuendesha majenereta yanayopoesha mifumo yake kwa siku 10 na kuzuia ajali za kinyuklia. Mitambo ya kinu hicho sharti ipoeshwe ili kuepusha kitisho cha janga la nyuklia.
(AFPE, DPAE,)
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Iddi Ssessanga