UN yataka ukanda salama kuwekwa Zaporizhzhia
7 Septemba 2022Kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia ambacho ndicho kikubwa zaidi barani Ulaya, kilianguka mikononi mwa wanajeshi wa Urusi mwezi Machi na kumekuwa na mashambulizi ya mara kwa mara karibu na eneo hilo, hali inayozusha hofu ya kutokea janga la nyuklia.
Shirika la Kimataifa la Kuidhibiti Nishati ya Atomiki – IAEA sasa limezihimiza Urusi na Ukraine kuweka kile linachokiita Ukanda wa ulinzi na usalama wa Nyuklia karibu na kinu hicho.
Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alitoaonyo kali kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, siku chache baada ya kuongoza ujumbe wa ukaguzi katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia. "Shambulizi lolote, iwe la kukusudia au kutokusudia, makombora ambayo kinu hiki kimepigwa, na hilo nilijionea binafsi na kutathmini, pamoja na watalaamu wangu, haikubaliki kabisa. Tunacheza na moto na jambo baya sana linaweza kutokea."
Katika mkutano huo wa Baraza la Usalama, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia aliwataka wanajeshi wa Urusi na Ukraine kukubaliana kuhusu ukanda usiokuwa na shughuli za kijeshi. Guterres amesema eneo la kinu cha Zaporizhzhia halipaswi kuwa jukwaa la operesheni za kijeshi. "Hiyo itajumuisha dhamira ya vikosi vya Urusi kuwaondoa wanajeshi wote na vifaa kutoka kwenye ukanda huo na dhamira ya vikosi vya Ukraine kutoingia katika eneo hilo."
Nini kilikuwa kwenye ripoti ya IAEA baada ya ziara ya Zaporizhzhia?
Katika ripoti kuhusu ziara yake, IAEA imesema mashambulizi ya makombora kwenye kinu hicho yanapaswa kusitishwa mara moja. Shirika hilo limesema hali hiyo inaleta hatari kubwa kwa usalama wa nyuklia.
Soma pia: Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wawasili Zaporizhzhia
Ripoti hiyo imesema hatua bora zaidi ya kuchukuliwa ni kusitishwa kwa vita, na kama hilo haliwezekani, basi eneo salama liwekwe. Aidha ilitoa wiro wa kuondolewa kwa magari ya kivita ya Urusi ambayo ujumbe wake uliyaona kiwandani hapo.
Je, ni uharibifu gani ambao wajumbe wa IAEA waliona?
Wakati wa ziara hiyo, IAEA ilisema iliona matukio mengi ya uharibifu, na kwa wakati mmoja ujumbe huo ulilazimika kujificha katika eneo salama kutokana na mashambulizi ya makombora.
Ripoti hiyo imewasifu wahudumu wanaokiendesha kinu hicho, lakini ikasema mazingira ya kazi na ya kuishi yanahitaji kuimarishwa ili waweze kuepuka hatari ya kutokea ajali ya nyuklia.
Kauli kuhusu ripoti hiyo
Katika Baraza la Usalama, Urusi imesema imesikitika kwamba ripoti hiyo haikuilaumu Ukraine kwa kufanya mashambulizi hayo. Balozi wa Urusi Vassily Nebenzia alikiambia kikao hicho kilichohudhuriwa kwa njia ya video na Grossi kuwa Urusi inaelewa nafasi ya IAEA kama mdhibiti wa kimataifa, lakini katika hali ya sasa ni muhimu kuyaelezea mambo kama yalivyo.
Urusi na Ukraine zinalaumiana kila mmoja kwa kushambulia eneo la kinu hicho, ambalo lilishambuliwa pia jana licha ya mapendekezo ya IAEA.
Nebenzia alisema kama uchokozi unaofanywa na utawala wa Kyiv utaendelea, hakuna hakikisho kuwa hapatakuwa na madhara, na wajibu wa hilo upo kabisa mikononi mwa Kyiv na waungaji mkono wake wa Magharibi na wanachama wengine wote wa Baraza la Usalama.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema amekaribisha ukweli kwamba ripoti hiyo ilibainisha uvamizi wa jeshi la Urusi katika kinu hicho. Alisema kama pendekezo la kuweka ukanda salama linalenga kuondoa shughuli za kijeshi kwenye eneo la kinu hicho, basi wanaliunga mkono.
dh/rt (AP, AFP, dpa)