IAEA kuweka ujumbe wa kudumu katika kinu cha Zaporizhzhia
2 Septemba 2022Hayo yametangazwa na mkuu wa shirika hilo, Rafael Grossi baada ya kukikagua kinu hicho hapo jana.
Rafael Grossi aliyabainisha hayo jana jioni baada ya kurejea katika maeneo yaliyo chini ya serikali ya Ukraine, baada ya kukikagua kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kwa masaa kadhaa.
Alisema ziara yake iliyowahusisha pia wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilitishiwa na milio ya silaha ambayo wakati mwingine ilikuwa karibu sana na mahali walipo.
IAEA kuweka ujumbe wa kudumu Zaporizhzhia
Akizungumza na vyombo vya habari, Grossi alisema ngwe ya kwanza ya ukaguzi iliyokuwa inasubiriwa kwa muda mrefu imemalizika, na kuongeza kuwa ujumbe wa shirika lake utasalia kwenye kinu cha Zaporozhzhia kwa hali ya kudumu.
''Nimehitimisha ziara ya kwanza muhimu ya ukaguzi, ambayo mara hii iliazimia kukitazama kinu chote,'' amesema Grossi, na kuongeza kuwa bila shaka yapo mengi zaidi ya kufanya, na ''la muhimu zaidi, tutaweka hapa ujumbe wa kudumu wa IAEA.''
Mkuu huyo wa shirika la IAEA alibainisha kuwa majengo ya kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia yalishambuliwa mara kadhaa, hali aliyoielezea kuwa ya kutia wasiwasi, na isiyopaswa kuendelae.
Alisema ataendelea kuhofia usalama wa wataalamu wa IAEA watakaokita kambi katika kinu hicho, hadi pale usalama utakapokuwa umetengamaa.
Nani anakishambulia kinu hicho cha nyuklia?
Kila upande katika mzozo huu wa vita, Urusi na Ukraine, unaulaumu mwingine kufanya mashambulizi hayo yaliyokilenga kinu hicho kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya.
Alipokitembelea kinu cha Zaporizhzhia Alhamisi, Grossi aliweza kuyafikia maeneo yote ya kinu hicho, zikiwemo sehemu nyeti kama mfumo wa dharura na chumba cha kuongozea shughuli zote.
Soma Zaidi: Putin kuruhusu wakaguzi kutembelea kinu cha nyuklia kinachodhibitwa na Urusi
Amesema wataalamu wa timu yake wanaosalia huko watakuwa na jukumu la kukamilisha uchunguzi na kufanya tathmini ya kiufundi.
Kinu cha Zaporizhzhia kinadhibitiwa na wanajeshi wa Urusi tangu mwanzoni mwa uvamizi wao nchini Ukraine, na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amerudia wito wake wa kutaka shughuli zote za kijeshi zikomeshwe katika mazingira ya kinu hicho, wito unaoungwa mkono na washirika wake wa magharibi pamoja na Umoja wa Mataifa.
-rtre, dpae