Umoja wa Mataifa waomba Sudan kuruhusu uingizwaji wa misaada
16 Machi 2024Waraka wa Umoja wa Mataifa ulioonwa na shirika la habari la AFP jana Ijumaa umeonyesha karibu raia milioni tano wa Sudan wanaweza kukabiliwa na uhaba wa chakula katika miezi ijayo.
Vita kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo, tangu Aprili mwaka jana vimeua maelfu ya raia, kuharibu miundombinu na kulemaza uchumi.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kiutu Martin Griffiths amesema karibu Wasudan milioni 18 tayari wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kuonya katika barua kwa Baraza la Usalama kwamba "takriban watu milioni 5 wanaweza kutumbukia katika janga hilo katika baadhi ya maeneo ya Sudan.
Mwakilishi wa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja huo, UNICEF, nchini Sudan, Mandeep O'Brien, amesema watoto milioni 14 wanahitaji misaada ya kiutu.