Watu kadhaa wauawa Haiti baada ya Gereza Kuu kuvamiwa
4 Machi 2024Mamia ya wafungwa pia wametoroka kutoka jela hiyo katika mwendelezo wa wimbi kubwa la machafuko linaloukumba mji mkuu wa taifa hilo la kanda ya Karibia.
Inaarifiwa watu watano wameuwawa kwenye mkasa huo wa siku ya Jumapili. Miili mitatu ya watu waliuwawa kwa kupigwa risasi imeonekana kwenye lango la kuingia kwenye jela hiyo ambalo liliachwa wazi bila kuwepo na maafisa wa ulinzi. Miili ya watu wengine wawili imeonekana barabarani.
Kuvamiwa kwa jela hiyo ni ishara nyingine ya kutanuka kwa hali ya machafuko nchini Haiti katika wakati magenge ya wahalifu yameongeza mashambulizi yake kwenye mji mkuu wa taifa hilo la kanda ya Karibia.
Hayo yametokea wakati Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry anafanya ziara nje ya nchi akijaribu kunusuru ahadi ya kutumwa kikosi cha Umoja wa Mataifa kwenda kusaidia kurejesha usalama kwenye taifa lake.
Maelfu ya wafungwa ikiwemo viongozi wa makundi ya uhalifu wanahofiwa kutoroka
Vurumai kwenye mji huo mkuu imepamba moto tangu Alhamisi ya wiki iliyopita huku makundi ya wahalifu wenye silaha yakisema yanalenga kuung´oa madarakani utawala wa Henry, ambaye analiongoza taifa hulo tangu kutokea mauaji ya rais Jovenel Moise mnamo mwaka 2021.
Mkuu wa Mtandao wa Kitaifa wa Kulinda Haki za Binadamu, Pierre Esperance, amesema ni wafungwa 100 pekee ndiyo wamesalia ndani ya gereza hilo lililokuwa na wafungwa wapatao 3,800.
"Tumehesabu miili mingi ya wafungwa," amesema Esperance. Mwandishi habari wa shirika la AFP aliyeitembelea jela hiyo jana Jumapili ameshuhudia miili kadhaa ya watu nje ya majengo ya gereza. Baddhi ilikuwa na vidonda vya risasi na vilipuzi vya aina nyingine.
Katika taarifa yake, serikali ya Haiti imesema polisi walijaribu kuzima shambulizi lililotokea kwenye jela hiyo pamoja na kwenye jengo lingine linaloitwa Croix des Bouquets.
Viongozi wa magenge ya wahalifu pamoja na wale walioshtakiwa kwa mauaji ya Moise ni miongoni mwa wale walikuwa wamefungwa kwenye gereza hilo, linalopatikana mita chake kutoka ikulu ya nchi hiyo.
Gazeti la kila siku la nchi Haiti la Le Nouvelliste limeripoti kwamba makundi ya wahalifu yalikuwa yakifanya ushushushu kwa kutumia droni tangu siku ya Alhamisi, kabla ya uvamizi uliotokea usiku wa kuamkia Jumapili.
Magenge ya uhalifu yanalenga kuuangusha utawala wa Ariel Henry
Kiongozi mwenye nguvu wa genge la uhalifu, Jimmy Cherisier, anayefahamika pia kwa jina la utani, Barbecue, amesema kupitia ujumbe wa video aloutuma kwenye mitandao ya kijamii kwamba, makundi yenye silaha ya Haiti yanashirikiana "kumshinikiza Waziri Mkuu Ariel Henry kuondoka madarakani."
Hadi sasa haijafahamika iwapo waziri mkuu huyo amerejea Haiti. Alikuwa ziarani nchini Kenya siku ya Ijumaa, kutafuta uungaji mkono wa kutumwa kikosi cha polisi cha kimataifa kwenda kuisaidia nchi yake.
Kenya ilikwishajitolea kuongoza kikosi hicho ambacho kiliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba mwaka jana.
Siku ya Ijumaa, waziri mkuu Henry alitia saini mkataba na serikali ya Kenya mbele ya Rais William Ruto ili kuwezesha kutumwa kwa kikosi hicho.
Hata hivyo mpango huo unakabiliwa na kihunzi kufuatia uamuzi uliotolewa na mahakama moja nchini Kenya mwezi Januari ambao umeipiga marufuku serikali kupeleka polisi nchini Haiti.
Haiti, taifa masikini zaidi kwenye kanda ya Karibia, imetumbukia kwenye mzozo kwa miaka kadhaa sasa na mauaji ya rais ya mnamo 2021 yamechochea zaidi machafuko.
Hakuna uchaguzi uliofanyika tangu mwaka 2016 na nafasi ya wadhifa wa rais bado iko wazi.