Watu 920 wafa kwa tetemko la ardhi Afghanistan
22 Juni 2022Akizungumza Jumatano na waandishi habari, Naibu Waziri wa Afghanistan anayehusika na majanga, Mawlawi Sharafuddin Muslim amethibitisha idadi hiyo ya vifo iliyotokana na tetemeko hilo la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 6.1 katika kipimo cha Richta. Tetemeko hilo la ardhi limelotokea kwenye majimbo ya Paktika na Khost
Aidha, naibu msemaji wa serikali ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban, Bilal Karimi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba tetemeko hilo limetokea kwenye wilaya nne za jimbo la Paktika.
Serikali ya Taliban yaomba msaada
Karimi ameyatolea wito mashirika ya misaada kupeleka wafanyakazi wake mara moja kwenye eneo la tukio ili kuzuia maafa zaidi.
Idara ya Hali ya Hewa ya nchi jirani ya Pakistan, imesema kuwa kitovu cha tetemeko hilo la ardhi kilikuwa katika jimbo la Paktika, karibu na eneo la mpaka na umbali wa kilomita 50 kusini magharibi mwa mji wa Khost. Shirika la habari la serikali Bakhtar limeripoti idadi hiyo ya vifo na mkurugenzi wake mkuu, Abdul Wahid Rayan ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba nyumba 90 zimeharibiwa katika jimbo la Paktika na watu kadhaa wanaaminika wamekwama katika vifusi.
Shirika linalohusika na matetemeko ya ardhi barani Ulaya, EMSC limesema kuwa matetemeko mengine madogo yamesikika umbali wa kilomita 500 kwa watu milioni 119 nchini Afghanistan, Pakistan na India.
Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoratibu msaada wa kibinaadamu, UNOCHA kimesema Afghanistan imeyaomba mashirika ya misaada ya kiutu kusaidia katika juhudi za uokozi. Msemaji katika wizara ya mambo ya nje ya Afghanistan amesema nchi hiyo inakaribisha misaada ya kimataifa. Nchi jirani ya Pakistan imesema inafanya kazi katika kuhakikisha inaongeza msaada.
Helikopta zapelekwa kwa ajili ya uokozi
Franz Marty, mwandishi habari aliyeko nchini Afghanistan, ameiambia DW kwamba helikopta zimepelekwa kusaidia katika juhudi za uokozi, kwani huchukua muda wa saa kadhaa kulifikia eneo hilo lililoko milimani kwa kutumia usafiri wa gari. Kwa mujibu wa Marty, madaktari wanaamini kuwa huenda idadi ya watu waliokufa ikawa kubwa zaidi kuliko iliyotangazwa rasmi.
Wakati huo huo, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewaombea wahanga wa tetemeko hilo la ardhi. Akizungumza Jumatano mbele ya waumini mjini Roma, katika viwanja vya kanisa la Mtakatifu Peter, Papa Frencis amesema anatoa salamu zake za pole kwa waliojeruhiwa na wale walioathiriwa na tetemeko hilo. Papa Francis amesema anawaombea wale waliowapoteza wapendwa wao pamoja na familia zao.
(DPA, AP, AFP)