1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watu waliokufa kwa tetemeko Nepal yafikia 3,700

27 Aprili 2015

Idadi ya watu waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi nchini Nepal, imefikia 3,700, huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa kutolewa msaada wa kimataifa na kuonya kuhusu mzozo wa kibinaadamu katika nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1FFQT
Eneo la mji wa Kathmandu baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi
Eneo la mji wa Kathmandu baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhiPicha: Reuters/N. Chitrakar

Taarifa zilizotolewa leo na serikali ya Nepal, zimeeleza kuwa idadi hiyo inaweza ikaongezeka zaidi kutokana na kuendelea zoezi la uokozi kwenye maeneo ya milimani ambako zoezi hilo linakabiliwa na mazingira magumu ikiwemo kukatika kwa mawasiliano, siku mbili baada ya kutokea tetemeko hilo lililokuwa na ukubwa wa kipimo cha richta 7.8.

Mkuu wa idara ya kushughulikia majanga ya kitaifa katika wizara ya mambo ya ndani ya Nepal, Rameshwor Dangal amesema zaidi ya watu 6,500 wamejeruhiwa katika tetemeko hilo. Dangal amesema watu wengine wapatao 81 wameripotiwa kufariki kutokana na tetemeko hilo ambalo limeziathiri pia nchi jirani zikiwemo India na China. Watu wengine 18 wamethibitika kufariki kutokana na maporomoko ya theluji kwenye Mlima Everest, kutokana na tetemeko hilo.

Asilimia 90 ya jeshi la Nepal linashiriki katika zoezi la uokozi, huku lengo lao kubwa likiwa kuwaokoa watu waliojeruhiwa. Zaidi ya vifo 1,000 vimetokea kwenye mji mkuu wa Nepal, Kathmandu. Maelfu ya familia wamelala nje ya nyumba zao kwa usiku wa pili huku wakiwa na hofu ya kutokea matetemeko mengine madogo.

Watu wakiwa wamelala mitaani baada ya tetemeko la ardhi
Watu wakiwa wamelala mitaani baada ya tetemeko la ardhiPicha: imago/Xinhua

Mratibu mkuu wa kiutawala wa Kathmandu, Ek Narayan Aryal, amesema mahema na maji leo yametolewa katika maeneo kumi ya mji huo, ambako kulikuwa na karibu matetemeko madogo 100, ambayo yanasababisha zoezi la uokozi kuwa gumu. Aryal amefafanua kwamba hali hiyo imekuwa ikisababisha pia hofu kwa wafanyakazi wa mashirika ya uokozi.

Hospitali zafurika watu

Umoja wa Mataifa umesema hospitali za Kathmandu zimefurika watu na zinapungukiwa vifaa vya huduma za dharura pamoja na ukosefu wa sehemu za kuhifadhia maiti. Hata hivyo, wakati misaada kutoka mataifa mbalimbali duniani ikianza kuingia nchini Nepal, wafanyakazi wa mashirika ya misaada wameonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi karibu na eneo la tukio.

Idara ya utafiti wa kijiolojia ya Marekani, imesema tetemeko hilo limeanzia karibu na wilaya ya Lamjung, iliyoko umbali wa kilomita 80 kaskazini-magharibi mwa Kathmandu. Misaada hiyo inatokea India, China, Pakistan, Marekani, Canada, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Poland, Italia, Korea ya Kusini, Israel na Singapore.

Akizungumzia kuhusu misaada, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Korea Kusini, Cho Tae-Yul anasema wako pamoja na Nepal, hivyo hawana budi kutoa ushirikiano. ''Kwa sababu mchakato wa kupitia misaada ya dharura na kutathmini ukubwa wa madhara huchukua muda mrefu, tumeamua mapema kupeleka timu ya wafanyakazi wa dharura,'' alisema Waziri Cho.

Wafanyakazi wa uokozi kutoka Japan wakiwasili Kathmandu
Wafanyakazi wa uokozi kutoka Japan wakiwasili KathmanduPicha: Jiji Press/AFP/Getty Images

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto-UNICEF, limesema karibu watoto milioni moja wanahitaji msaada wa dharura kutokana na tetemeko hilo la ardhi. Msemaji wa UNICEF, Christopher Tidey, amesema wafanyakazi wa shirika hilo wanapambana kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kwa watoto.

Aidha, shirika la kimataifa la kutoa misaada OXFAM limetoa wito wa kutolewa msaada wa haraka pamoja na kuwepo kwa mikakati ya muda mrefu ili kukabiliana na mzozo huo na kuepusha umaskini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu