Tetemeko kubwa Nepal dunia yatoa msaada
26 Aprili 2015Pamoja na hayo mashirika ya kutoa misaada yana wanawasi wasi juu ya uhakika wa kuwafikia watu walionusurika na maafa hayo.
Zaidi ya watu 1,800 wamethibitishwa kuwa wamefariki na wengine wengi wanahofiwa wamenaswa chini ya kifusi katika tetemeko hilo la ardhi baya kabisa kuwahi kutokea nchini humo kwa zaidi ya miaka 80.
Wakati mawasiliano ya internet na simu za mkononi yamekatika na barabara nyingi zilizoharibika zimefungwa, dunia imekuwa ikihangaika kupata picha kamili ya kile ambacho kinahitaji haraka kufuatia tetemeko hilo la ardhi lililofikia katika kipimo cha 7.8 lililotokea jana Jumamosi(25.04.2015).
Wanatambua wanahitaji kuharakisha. Uwanja wa ndege wa Kathmandu umefunguliwa tena , ikiwa hii ni hatua muhimu .
"Tunafahamu uharibifu ni mkubwa na kwamba kuyafikia maeneo ya ndani itakuwa vigumu sana kwa kila mtu," amesema Ben Pickering, mshauri wa shirika la Save the Children nchini Uingereza. "Watoto wataathirika kwa njia nyingi. Kuumia. Kutengana na familia."
Shirika la Madaktari wasio na mipaka limesema vikosi vinne vinaondoka leo Jumapili(26.04.2015)asubuhi kwenda Nepal kutoka jimbo la Bihar nchini India, jimbo lililoko karibu na mpaka na Nepal.
Mashirika yameanza kutoa misaada
Shirika la makaazi kwa binadamu duniani , Habitat for Humanity International ambalo limefanyakazi nchini Nepal kwa miaka kadhaa, limesema litaanza mara moja usambazaji wa vifaa 20,000 vya hifadhi ya malazi wakati likitathmini kiwango cha uharibifu na kutayarisha mipango ya ujenzi.
Shirika la AmeriCares limetuma kikosi kutoka India na linatayarisha shehena ya msaada wa madawa pamoja na misaada mingine. Shirika la Handicap International , ambalo lina wafanyakazi 47 ndani ya nepal kabla ya tetemeko hilo, limekuwa tayari likijishughulisha na misaada ya dharura.
Shirika la Ufaransa la madaktari wa dunia , Medecins du Monde, limesema linakusanya wafanyakazi wake nchini Nepal na linatuma wafanyakazi wengi zaidi pamoja na msaada wa madawa katika eneo hilo haraka.
Mercy Corps limesema linaangalia usalama wa kundi kubwa la wafanyakazi wake ambao tayari wako nchini humo na wanatathmini hali ilivyo.
China na Marekani zasaidia
Kikosi chenye watu 62 cha utafutaji wa watu na uokozi kutoka China , pamoja na mbwa sita, kinatarajiwa kuwasili Kathmandu mchana leo Jumapili(26.04.2015) kwa ndege ya kukodi, shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya China Xinhua limeripoti, likinukuu idara ya kushughulikia tetemeko la ardhi nchini China.
Ubalozi wa Marekani nchini Nepal umetangaza msaada wa awali wa dola milioni 1, na idara ya maendeleo ya kimataifa ya Marekani imeanzisha msako katika miji pamoja na kikosi cha uokozi.
Umoja wa Ulaya unatafakari , kupanga msaada wa bajeti kwa Nepal, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja kati ya mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya , na kamishna wa maendeleo na wa masuala ya kiutu.
Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki Papa Francis amesema amesikitishwa mno na tetemeko hilo kubwa ambalo limeuwa zaidi ya watu 1,800 nchini Nepal na kueleza mshikamano wake na wale walioathirika na mkasa huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae
Mhariri: Abdu Mtullya