1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 71 wauawa katika mashambulizi kusini, katikati mwa Gaza

23 Februari 2024

Mashambuzi ya Israel yamelenga makaazi kusini na katikati mwa Gaza huku wizara ya afya ya ukanda huo ikisema mashambulizi hayo yameua takriban watu 71, na kuongezea juu ya hali inayotajwa na mashirika ya misaa kuwa mbaya

https://p.dw.com/p/4cnBD
Ukanda wa Gaza | Uharibifu katika Rafah
Wapalestina wakiangalia uharibifu baada ya Israel kushambulia majengo ya makazi na msikiti huko Rafah, Ukanda wa Gaza, Alhamisi, Februari. 22, 2024Picha: Hatem Ali/AP Photo/picture alliance

Taarifa ya Alhamis ya wizara ya hiyo iliyo chini ya wapiganaji wa Hamas, imesema vifo vyote hivyo 71 vimetokea katika mapigano yalidumu kwa takribani masaa 24 yaliopita. Wakati huohuo, mvutano unaripotiwa kuongezeka kwenye eneo linalokaliwa kibamavu na Israel la Ukingo wa Magharibi, ambapo watu watatu wenye silaha walifyatua risasi  Asubuhi ya Alhamis kwenye barabara karibu na kituo cha ukaguzi, na kuua Muisraeli mmoja nakujeruhi polisi wasiopungua watano.

Polisi ya Israel imesema washambuliaji wawili waliuwawa katika eneo la tukio. Na yule wa tatu alikamatwa baadae na kuwekwa kizuizini. Kwa upande wao wanadiplomasia wa Ulaya wanaongeza wito wa kusitisha mapigano, ikiwa ishara ya wazi kuwa  mzozo wa kibinadamu unaozidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza.

Hali ngumu katika eneo la Ukanda wa Gaza

Nour Hamad ambae ni mkazi wa Rafah anasema "Hakuna sehemu salama katika Gaza, walisema Rafah ni eneo salama, tazama na uwaonyeshe watu jinsi hali ilivyo. Je, kuna usalama gani? Walifyatua mabomu kwa watu wasio na hatia wakiwa usingizini. Hawakuwa na hatia. Watoto waliachwa kwenye majengo yaliporomoka usiku wa  jana."

Ukanda wa Gaza | Uharibifu katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia
Mpalestina akitundika nguo karibu na jengo lililoharibiwa, katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza Februari 22, 2024.Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Katika muendelezo wa juhudi za kusitisha mapigano, kundi la Hamas limesema kiongozi wake Ismail Haniyeh, ameondoka Misri baada ya kufanya mazungumzo na maafisa wa Misri kuhusu uwezekano wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo hao na wafungwa wa Kipalestina ambao wapo katika magereza ya Israel.

Tangazo la ujenzi wa nyumba 3, 300 katika eneo la walowezi

Ndani Isreal waziri kutoka katika upande wa mrengo mkali wa kulia, Bezalel Smotrich ametangaza hatua nyingine ya taifa lake ya kupanga kuidhinisha ujenzi wa zaidi ya nyumba mpya 3,300 katikaeneo la walowezi la Ukingo wa Magharibi.

Kuidhinishwa kwa ujenzi mpya kunabashiriwa kuibua lawama kutoka kwa Marekani wakati ambapo uhusiano kati ya mataifa hayo washirika hauko sawa kutokana na kutolewana katika muelekeo wa vita ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa yake ya jioni ya Alhamis waziri huyo amesema matokeo yalisukumwa na mashambulizi ya risasi ya Wapalestina ya karibu na mji wa Jerusalem mapema jana. Aidha ameongeza kuwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant walishiriki katika mjadala huo ulioridhia uamuzi wa ujenzi.

Soma zaidi:Israel yafanya mashambulizi huko Rafah

Vita vya Gaza vilianza baada ya tukio la Oktoba 7 la wanamgambo wa Hamas kuvamia kusini mwa Israel na kuwaua watu wapatao 1,200 na kuwachukua wengine karibu mateka 250. Lakini takriban mateka 130 ambao ambao wanashikiliwa na wanamgambo wa Hamas, na inaaminika uwenda wakawa wamekufa.

Wizara ya Afya ya Gaza inakadiria zaidi ya Wapalestina 29,000 wameuwawa tangu kuzuka kwa vita hivyo.