Israel yaishambulia Gaza baada ya turufu ya Marekani UM
21 Februari 2024Katika hali inayozidisha masaibu ya Gaza, shirika la chakula la Umoja wa Mataifa lilisema Jumanne kwamba limelaazimika kusitisha upelekaji wa mahitaji muhimu kaskazini mwa eneo hilo baada ya kukabiliwa na machafuko na vurugu huko -- uamuzi uliolaaniwa na Hamas.
Siku ya Jumapili, shirika hilo la Mpango wa Chakula Duniani ndiyo lilikuwa limeanza tu kusambaza tena mahitaj mhimu lakini lilisema msafara wake ulikumbana na mashambulizi ya risasi, vurugu na uporaji, huku dereva wa lori akipigwa.
Ofisi ya habari ya serikali ya Hamas imeeleza kushtushwa na uamuzi huo wa WFP kupeleka msaada wa chakula Gaza Kaskazini, hali walioitafsiri kama hukumu ya kifo kwa theluthi tatu ya watu milioni moja.
Ikilitolea wito shirika hilo kubadili uamuzi huo mara moja, ofisi hiyo ilisema wanaubebesha dhamana Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kwa matokeo ya uamuzi huo.
Tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas, Gaza imetumbukia katika mgogoro wa chakula, huku misaada kutoka nje ikiwekewa vikwazo vikali.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukitoa tahadhari ya mara kwa mara juu ya hali mbaya ya kibinadamu Gaza, na kuonya kwamba uhaba wa chakula unaweza kusababisha "mlipuko" wa vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika.
Soma piaVita vya Israel-Hamas vyazua mvutano tamasha la Berlinale:
Mapigano yasiyokoma yaliodumu kwa zaidi ya miezi minne yameteketeza sehemu kubwa ya eneo hilo la pwani, na kuwasukuma watu milioni 2.2 kwenye ukingo wa njaa na kusababisha robo tatu ya watu kuyahama makazi yao, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.
"Hatuwezi kuvumilia tena. Hatuna unga, hatujui hata wapi pa kwenda katika hali hii ya baridi," alisema Ahmad, mkazi wa mji wa Gaza, ambapo mitaa imetapakaa vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na takataka.
"Tunataka usitishaji mapigano. Tunataka kuishi," alisema
Marekani yanyooshewa kidole kuendelea kwa vita
Lakini mjini New York, Marekani ilipinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoandaliwa na Algeria, ambalo lilitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa misingi ya kibinadamu na kuachiliwa bila masharti kwa mateka wote waliochukuliwa katika mashambulizi ya Oktoba 7.
Linda Thomas-Greenfield, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, aliitaja kura hiyo kuwa isiyo na mashiko na kudai inaweza kuhatarisha mazungumzi ya kuwachiwa mateka.
Kura hiyo ya turufu iliibua shutuma kutoka kwa nchi zikiwemo China, Urusi, Saudi Arabia na hata washirika wa karibu wa Marekani Ufaransa na Slovenia, huku China ikionya Jumatano kwamba uamuzi huo wa Marekani umeusukuma mzozo huo katika hali ya hatari zaidi.
"China ilipiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio hilo," msemaji wa wizara ya mambo ya nje Mao Ning aliuambia mkutano wa kawaida Jumatano.
"Marekani kwa mara nyingine tena imepiga kura ya turufu peke yake, na kusukuma hali ya Gaza kuwa ya hatari zaidi, ambapo pande zote zinazohusika... zimeelezea kusikitishwa kwao na kutoridhika kwao," aliongeza.
Soma: Kiongozi wa Hamas awasili Cairo kujadili hali ya Gaza
"Hali ya kibinadamu huko Gaza inazidi kuwa mbaya, na amani na utulivu wa kikanda vimeathiriwa sana," Mao alisema. "Baraza la Usalama lazima lichukue hatua haraka iwezekanavyo ili kusimamisha uhasama. Hili ni jukumu la kimaadili ambalo haliwezi kuahirishwa," alisema.
"Tutaendelea kufanya kazi na pande zote katika jumuiya ya kimataifa kusukuma Baraza la Usalama kuchukua hatua zaidi za kuwajibika na zenye maana, na kufanya juhudi zisizo na kikomo kuzima vita huko Gaza mapema," Mao aliongeza.
Hamas ilisema kura ya turufu ya Marekani ni sawa na "taa ya kijani kwa majeshi ya ukaliaji kufanya mauaji zaidi".
Vifo zaidi ya 100 baada ya kurua ya turufu ya Marekani
Baada ya kura hiyo ya baraza la Usalama, Israel iliishambulia Gaza mapema leo huku mapigano yakiendelea, na kusababisha vifo vya watu 103, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas katika eneo hilo.
Mashuhuda wameripoti moto mkubwa katika maeneo yanayozunguka Gaza, ikiwemo miji ya kusini ya Khan Yunis na Rafah, karibu na mpaka wa Misri, ambapo karibu Wapalestina milioni 1.4 waliokimbia makaazi yao wametafuta hifadhi.
Soma pia: Israel yaitwanga Gaza kabla ya kura ya usitishaji vita UM
Rafah, mji wa mwisho wa Gaza kukabiliwa na uvamizi wa ardhini na wanajeshi wa ardhini wa Israel, pia ni kitovu kikuu cha msaada unaohitajika sana kupitia Misri.
Qatar, ambayo imekuwa na jukumu muhimu katika juhudi za upatanishi kati ya Hamas na Israel, ilisema Jumanne kwamba dawa zilizotumwa Gaza chini ya makubaliano yaliyojadiliwa kwa pamoja na Ufaransa zimewafikia mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo hao, kwa kubadilishana na shehena ya misaada ya kibinadamu.
Lakini kwa ujumla, juhudi za mazungumzo zimeshindwa kupata mwafaka wa muda mrefu na licha ya shinikizo la kimataifa, Israel imesisitiza kuwa operesheni ya ardhini Rafah ni muhimu kuisambaratisha Hamas.