Kipi kitaishawishi Misri kufungua mipaka kwa Wapalestina?
19 Februari 2024Wiki iliyopita, jeshi la Israel lilisema litafanya mashambulizi kwenye mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza, karibu na mpaka wa Misri, ambako zaidi ya Wapalestina milioni 1 wamekimbilia kutafuta hifadhi.
Taasisi ya Usalama wa Kitaifa na Mkakati wa Wazayuni ya Misgav, imetoa ripoti inayosema kuwa mzozo huo ni "fursa ya kipekee na adimu ya kuwahamisha wakaazi wote wa Ukanda wa Gaza."
Mpango huo ulioripotiwa ni jambo ambalo serikali ya Misri imelipinga vikali, ikihofia kwamba Wapalestina wanaoondoka hawataruhusiwa kurudi. Wakati huo huo, uamuzi utatolewa hivi karibuni na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kuhusu iwapo Misri itapata nyongeza ya mkopo kuinua uchumi wake unaokabiliwa na madeni makubwa pamoja na sarafu yake inayofifia.
Je huu ni usaliti?" Habari ya hivi karibuni ya gazeti la mtandaoni linalomilikiwa na Lebanon la Al Modon liliuliza, likikisia kwamba Misri inaweza kusamehewa madeni yake ya kimataifa na wadau wakuu wa IMF nchini Marekani na Ulaya ikiwa itawapokea Wapalestina walioyakimbia makaazi yao.
Muda wa kutolewa kwa ripoti hiyo na nyingine za awali ikiwa ni pamoja na gazeti la Financial Times la Uingereza ambalo limesema wanasiasa wa Israel wamewataka washirika wao wa Ulaya kuishinikiza Misri kufungua mipaka unaonekana kuhalalisha tuhuma hizo.
Soma pia:Blinken akutana na El-Sisi kujadili mzozo wa Gaza
Hatua hiyo pia ina mfano. Mnamo mwaka 1991, Marekani iliisamehe Misri karibu dola bilioni 10 za deni lake kwa sababu ilikubali kuunga mkono muungano unaoongozwa na Marekani kuivamia Iraq.
Lakini katika hali hii, hilo silo linalofanyika. Riccardo Fabiani, mkurugenzi wa mradi wa Afrika Kaskazini wa shirika lisilo la kiserikali la International Crisis Group, ameiambia DW kuwa uvumi huu umekuwa ukienea nchini Misri kwa muda mrefu sasa tangu Oktoba 7.
"Ilikuwa hali ya kawaida sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini pia mitaani, watu wakisema kuwa nchi za Magharibi zinatoa pesa kwa Misri kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi''.
Lakini, Fabiani ameongeza kuwa kuna hali ya sintofahamu. IMF, Umoja wa Ulaya na kwa ujumla zaidi, mataifa ya Magharibi, yako tayari na yamejiandaa kutoa pesa kwa Misri kwa sababu yana wasiwasi mkubwa kuhusu kuyumba kwa nchi hiyo kwa sababu ya mzozo wa Gaza.
Kwa sasa, serikali ya kimabavu ya Misri inajikokota katikati ya hisia za watu wengi. Idadi kubwa ya watu inaunga mkono suala la Palestina na mipango ya muda mrefu ya usalama na Israel.
Wataalamu wote ambao DW ilizungumza nao walikubaliana kwamba kitakachofuata katika mpaka wa Misri na Gaza kinategemea zaidi Israel.
Wapalestina kuihama kabisa Gaza?
Taarifa fupi iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Januari na shirika hilo la International Crisis Group, imesema wanadiplomasia wa Misri, wanaendelea kushuku kuwa lengo lililofichwa la Israel ni kuwasukuma Wapalestina kuelekea mpaka wa Misri, na kwamba Wapalestina wanaweza hata kujaribu kuingia Sinai kwa hiari yao wenyewe ikiwa hatua za Israeli zitafanya hali katika Ukanda wa Gaza kuwa ngumu zaidi.
Ashraf Hassan wa shirika la Century International amesema kuwa hili litakuwa tukio baya zaidi kwa sababu hakutakuwa na suluhisho la mazungumzo
"Nadhani kwa hakika, Israel huenda ikajaribu kutumia mgogoro huu wa kiuchumi kuishinikiza Misri kufungua mpaka wake ili kufikia lengo la muungano wa mrengo wa kulia unaoongoza nchini Israel, ambao kimsingi ni kupunguza idadi ya watu katika Ukanda wa Gaza.''
Soma pia:Hamas yazingatia pendekezo la mapatano lililoridhiwa na Israel
Mirette Mabrouk, mkurugenzi mwanzilishi wa taasisi ya Mashariki ya Kati kuhusu mpango wa Misri yenye makao yake mjini Washington, amesema kwamba katika kiwango hicho hakuna chaguzi nyingi na kwamba iwapo Wapalestina watavuuka mpaka, Misri itawapokea kwa sababu haiwezi kuanza kuwapiga risasi wanawake na watoto wanaohangaika.
Mabrouk amemaliza kwa kusema kuwa tatizo la kuuliza mtu yeyote kutabiri nini kitafuata huko Rafah ni kwamba yote yatategemea kile ambacho Waisraeli watakifanya baadaye, kwani hakuna mtu anayewawajibisha, akiongeza kwamba watu wengine wowote wanabakia kutoa hisia na maoni yao tu.