1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMali

Watu 64 wauawa Mali kwenye mashambulizi tofauti

Sylvia Mwehozi
8 Septemba 2023

Watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wamefanya mashambulizi kwenye kambi ya kijeshi na boti ya abiria kaskazini mwa Mali na kuwaua watu 64.

https://p.dw.com/p/4W5hK
Mali | Soldat mit Ak-47
Picha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP/Getty Images

Mamlaka ya kijeshi nchini Mali, zimesema kuwa shambulizi moja liliilenga boti ya abiria katika mji wa Timbuktu katika mto Niger na jingine kwenye kambi ya kijeshi ya Bamba inayopatikana katika mkoa wa kaskazini wa Gao na kuwaua raia 49 na askari 15.

Boti ya abiria ilikuwa ikipitia njia iliyoanzishwa kati ya miji kando ya mto na ilishambuliwa kwa maroketi matatu ambayo yalizilenga injini zake. Kundi moja lenye mafungamano na kundi la Al-qaeda limedai kuhusika na mashambulizi yote mawili. Serikali ya Mali imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo. Mto Niger ni kiungo muhimu cha usafiri katika eneo ambalo miundombinu ya barabara ni duni.Wanajeshi 17 wa Niger wauawa katika shambulizi karibu na Mali

Mali
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius mjini Gao MaliPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kwenye tangazo lake, serikali ya Mali imesema vikosi vyake vimewaua pia wapiganaji takribani 50. Tangu mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka uliopita makundi yaliyo na silaha yamekuwa yakiuzuia mji wa Timbuktu baaada ya jeshi la Mali kupeleka vikosi vyake katika eneo hilo. Waasi wanazuia jiji hilo la jangwa kutouziwa bidhaa za msingi. Zaidi ya wakaazi 30,000 wameukimbia mji huo na eneo jirani, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya kiutu.

Mashambulizi hayo yametokea wakati Umoja wa Mataifa ukijiandaa kuondoa ujumbe wake wa askari 17,000 wa kulinda amani MINUSMA kutoka Mali kufuatia ombi la utawala mpya wa kijeshi. Zoezi hilo limepangwa kukamilika mwisho wa mwaka.

Mali imepambana kuzuia uasi wa wapiganaji wa Kiislamu walio na itikadi kali tangu mwaka 2012. Waasi hao walilazimishwa kuondoka madarakani katika miji ya kaskazini mwa Mali mwaka uliofuata katika operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Ufaransa lakini walijikusanya tena jangwani na kuanzisha mashambulizi dhidi ya jeshi la Mali na washirika wake. Mali imekuwa na mapinduzi mawili tangu mwaka 2020ambapo jeshi liliapa kukomesha uasi.